*Kampeni zake zagusa maelfu ya wananchi
Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kudhihirisha kwa vitendo namna ambavyo kinakubalika nchini ambapo maelfu ya wananchi wameendelea kujitokeza katika mikutano yake ya kampeni inayoendelea kufanyika maeneo mbalimbali nchini.
Hali hiyo ni matokeo ya utekelezaji Ilani ya Uchaguzi (2020 – 2025) kwa mafanikio ambayo Watanzania wameyashuhudia katika sekta za afya, elimu, maji, miundombinu na utawala bora.
Mgombea Urais kupitia CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan tayari ameshafanya mikutano yake ya kampeni katika mikoa ya Morogoro, Dododoma na Songwe ambako aliwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka mitano kisha kutoa ahadi mbalimbali zenye lengo la kuboresha maisha ya Watanzania kama ilivyokuwa kauli mbiu ya Chama katika uchaguzi huo isemayo ‘Kazi na Utu, Tunasonga mbele.’
Akiwa mkoani Dodoma, Dk. Samia alihutubia wananchi Kibaigwa wilayani Kongwa, Chamwino, Chemba, Kondoa kisha kishindo kikuu kuhitimishwa ndani ya Jiji la Dodoma ambako mafuriko ya watu yalitawala katika viwanja vya Tambukareli huku viongozi mbalimbali wakiungana na Dk. Samia kuwaomba wananchi kura zote kwa wagombea wa CCM.
Viongozi hao ni Waziri Mkuu Mstaafu na Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Mzee John Samweli Malecela, Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Mzee Philip Mangula na Katibu Mkuu mstaafu wa Chama, Balozi Dk. Bashiru Ali.
Akihutubia wananchi katika mkutano huo, Rais Dk. Samia alisema wananchi wa Dodoma wamethibitisha mkoa huo ndiyo makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi.

Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuchapakazi huku akieleza mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wake.
“Awamu ya tano tulifanya maamuzi ya kuhamia Dodoma, awamu ya sita tumekwenda kuendeleza kuhamia Dodoma, taasisi zote za serikali zipo Dodoma, maamuzi yote makubwa sasa yanafanyika hapa.
Aliongeza: “Tumemimina sh. trilioni 9.5 kwa miradi 3,093 ndani ya Mkoa wa Dodoma, mbali na kuongeza majengo na kuipa hadhi Hospitali ya Benjamin Mkapa, wilaya za Dodoma zina hospitali za kisasa ambazo vipimo vyote vinapatikana huko,” alisema.
Pia, Dk. Samia alisema serikali yake imejitahidi kufungua fursa za ajira kupitia uwekezaji kwa kujenga viwanda, kutengeneza fursa kwa wafanyabiashara wadogo huku mradi wa reli ya kisasa (SGR) ukiongeza kasi ya ukuaji uchumi.
Kuhusu umeme, alisema serikali inandelea na kazi ya kumalizia vitongoji ili kila mtu apate nishati hiyo kufanyakazi na kulinda usalama wao.
Kadhalika, alisema Chama kimejipanga kutatua uhaba wa maji kwa kutekeleza mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria na kumalizia ujenzi bwawa la Farkwa kusaidia kuleta maji Dodoma.

“Umeme wakati mwingine ni mdogo, tumejipanga kujenga njia kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma ili tupate umeme mkubwa wa kilovoti 400. Tuifanye Dodoma iwe ya viwanda, kazi zote zisisimame kwa sababu ya umeme,” alieleza.
Vilevile, alitoa ahadi ya kuongeza kasi ya upimaji na usajili ardhi ili kutatua migogoro, kukamilisha ujenzi wa kiwanja kikubwa cha mpira wa miguu ambapo tayari mkandarasi ameshapatikana.
Akiwa wilayani Chemba, Rais Dk. Samia alitoa ahadi ya ujenzi wa barabara Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma ikiwemo barabara ya Chemba – Soya yenye urefu wa kilometa 32.
Alieleza kuwa barabara hiyo imekuwa ikilalamikiwa na wananchi kwa muda mrefu, hivyo ahadi yake ni kwamba inaenda kutengenezwa kwa kiwango ambacho itakuwa inapitika msimu wote.
“Barabara hiyo ya Chemba – Soya ni tegemeo kwa shughuli za minada inayofanyika kila Jumapili ambayo inaingiza kiasi kikubwa cha fedha ndani ya halmashauri lakini na wafanyabiashara wadogo na wafugaji wanaitegemea kwa kiuchumi,” alieleza.
Akizungumza barabara ya Kwamotoro – Mpende – Kasakai – Ilahoda na zingine tatu za ndani ya wilaya hiyo, aliahidi kuangalia uwezekano Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini(TARURA) kuiboresha ili itumike katika kipindi chote.
Pia, alisema ipo barabara ya Tanga – Handeni – Kiberashi ambayo wamemaliza upembuzi yakinifu na utekelezaji wake utaanza mwaka huu huku akisisitiza barabara hiyo inakwenda kujengwa.

“Lakini kuna ahadi nyingine aliyoitoa mpendwa wetu Dk. Magufuli ya kujenga soko na stendi ndani ya Mji wa Chemba, hii nayo tunakwenda kuifanyia kazi kuhakikisha tunamaliza adha hii ya soko na stendi. Kwa upande wa ujenzi wa bwawa la Farkwa unaendelea vizuri nasi tutaendelea kuhakikisha linamalizika.
“Kwasababu tunalitegemea kwa Mji wa Dodoma ambao sasa ni mji mkubwa wa nchi yetu, uhamiaji umeongezeka, mahitaji ya maji ni makubwa mno. Bwawa kama hili ndilo litakalotuokoa, tutahakikisha linamalizika ili tupate maji ya kutosha ndani ya Mji wa Dodoma,” alibainisha.


