Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameelekeza kuwa maafisa na watumishi wa ofisi yake atakaoambatana nao katika safari zake za kikazi watatumia usafiri wa pamoja ili kubana matumizi ya nishati ya mafuta.

“Nimeanza kwa upande wangu; kuanzia sasa, ninaposafiri, watendaji wa ofisi yangu nitakaoambatana nao watatumia usafiri wa pamoja wa mabasi madogo ili kupunguza matumizi ya mafuta na gharama za uendeshaji katika kipindi hiki,” amesema Rais Dkt. Samia.

Aidha, amezitaka Wizara na Taasisi nyingine za Serikali kuchukua hatua za kupunguza matumizi ya mafuta katika kipindi hiki.

Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni.

Viongozi walioapishwa ni: Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu); Mhe. Dkt. Festo John Dugange kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI (Masuala ya Elimu); Mhe. Reuben Nhamanilo Kwagilwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira); na Mhe. Gerson Mdemu, Jaji wa Mahakama ya Rufani kuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Rais Dkt. Samia amesema vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati vimeathiri nchi nyingi duniani, ikiwemo Tanzania, kutokana na kupanda kwa bei za mafuta na bidhaa.

Ameongeza kuwa, bei za mafuta zimefikia viwango vya juu katika baadhi ya nchi, hali iliyosababisha nchi hizo kupunguza shughuli za kiuchumi zinazotegemea matumizi ya Nishati ya Mafuta.

Halikadhalika, amebainisha pamoja na kuwa Tanzania imekumbwa na athari hizo, bado ipo katika hali nafuu ya upatikanaji na hata bei za mafuta ikilinganishwa na nchi nyingine. Vilevile, amebainisha kuwa Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya upatikanaji wa mafuta nchini, na kuongeza kuwa nchi ina akiba ya mafuta inayotosheleza matumizi ya takribani miezi mitatu.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wafanyabiashara nchini kutochukua fursa ya kupanda kwa bei za mafuta kupandisha bei za bidhaa kiholela, hususan kwa bidhaa ambazo tayari zipo maghalani.

Vion