Kwa miaka mingi, Tanzania imekuwa kisiwa cha amani katika bahari yenye misukosuko ya migogoro barani Afrika. Tulijenga taifa letu juu ya misingi ya haki, utu, na umoja. Hizi ni tunu ambazo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliziita nguzo za uhai wa taifa.
Lakini leo, nchi yetu iko katika kipindi kigumu cha majaribu ya kisiasa, kijamii na kimaadili. Wapo wanaosema “amani ipo,” lakini ukweli ni kuwa mioyo ya wananchi wengi imejaa huzuni, hofu na shaka. Wapo waliopoteza ndugu zao, wapo wanaoteseka kwa majeraha, na wapo waliopoteza imani kwa taasisi za nchi yetu.
Taasisi kama Polisi inatazamwa vibaya na wananchi, lakini kwa watawala imekuwa mhimili wa nguzo inayolinda utawala wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi.
Nani sasa anaweza kutilia shaka ripoti ya Tume ya Haki Jinai ya mwaka 2023 iliyoongozwa na Jaji Othman Chande? Tume ilisema haya: “Taswira ya Jeshi la Polisi: Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusu vitendo vinavyochafua taswira ya Jeshi la Polisi.
“Malalamiko hayo dhidi ya Jeshi la Polisi yanahusu kushindwa kuzuia uhalifu, matumizi ya nguvu kupita kiasi, kubambikia kesi, vitendo vya rushwa, mali za watuhumiwa kupotea vituoni na kuchelewa kufika kwenye maeneo ya matukio. Hali hiyo inasababisha wananchi kupoteza imani kwa Jeshi la Polisi na kutokutoa ushirikiano unaotakiwa.
“Tume inapendekeza:
(i) Jeshi la Polisi lifanyiwe tathmini ya kina itakayowezesha Jeshi hilo kufanyiwa maboresho makubwa na kuundwa upya ili kuondoa kasoro za kiutendaji zilizopo;
(ii) Jeshi la Polisi libadilishwe kisheria, kimuundo na kifikra na kuwa Polisi Tanzania (National Police Service) ili kutoa taswira kuwa Jeshi la Polisi ni chombo cha kuwahudumia wananchi;
(iii) Kubadilisha mitaala ya mafunzo na mtazamo wa askari wa Jeshi la Polisi ili kutoka katika dhana ya ujeshi (police force) kwenda dhana ya kuhudumia wananchi (police service);
(iv) Jeshi la Polisi liboreshe mfumo wa ndani wa kushughulikia malalamiko ya wananchi; na
(v) Jeshi la Polisi liimarishe huduma za Intelijensia ya jinai na Polisi Jamii na kuanzisha programu za kuisogeza zaidi kwenye jamii.”
Haya ni maneno ya Tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan mwenyewe. Je, baada ya hiki kilichoonekana Oktoba 29, bado Rais ana kigugumizi cha kutekeleza ushauri wa Tume yake? Tuache kuwa nchi ya ripoti na maneno mengi, wananchi wanataka vitendo.
Maumivu ya Watanzania hayawezi kuponywa kwa kauli za kisiasa pekee, bali kwa v8itendo vya dhati, vya kiutu na vya haki.

Hapa nigusie huu msamiati wa “maridhiano”. Hili ni neno zuri. Linavutia. Lakini lina maana tu pale ambako haki inatendeka. Wakati Rais Samia anapozungumzia maridhiano ya kitaifa, wananchi wengi wanajiuliza: “Tutafanya maridhiano kuhusu nini, kama hatujui kilichotuumiza?”
Kabla ya kuzungumza kuhusu maridhiano, taifa lina wajibu wa kwanza wa kukubiliana na ukweli. Kwa maana hiyo, ni muhimu kuunda Tume Huru, hasa Tume ya Majaji na wazalendo wengine kuchunguza kwa kina chanzo cha maandamano, vurugu na mauaji ya kutisha yaliyotokea kuanzia Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali nchini.
Tume itatueleza kama ni kweli wauji walikuwa maharamia kutoka nje, na kama ni kweli walipenya, hali hiyo inaviweka wapi vyombo vyetu vya ulinzi na usalama? Bado akili ya kawaida kabisa inagoma kukubali kuwa wauaji walitoka nje! Asanteni sana JWTZ kwa kazi iliyotukuka. Kwa maelezo ya wananchi walionusurika, mmeokoa roho za Watanzania wengi mno. Hii ndiyo maana halisi ya Jeshi la Wananchi!
Tume ninayopendekeza hapa, iwe na mamlaka ya kuita mashahidi, kuhoji vyombo vya usalama, na kutoa mapendekezo yatakayosaidia taifa kuepuka makosa kama hayo kutendwa siku zijazo. Ripoti yake iwe wazi kwa umma. Kukiri makosa si udhaifu; bali ni ujasiri na tiba kwa migogoro ya kitaifa.
Tukio la mauaji, majeruhi na uharibifu wa mali limeacha kovu kubwa mno kwa maisha ya Watanzania na heshima ya nchi. Binafsi sikutarajia Tanzania ingekuwa ile ya Oktoba 29. Bila shaka wengi tuliamini hivyo, ingawa mara kadhaa tulionywa kuwa hatuna tofauti na walimwengu wengine wanaouana. Wapo watoto walioachwa yatima, wake waliopoteza waume zao, wazazi waliopoteza vijana, na kadhalika.
Serikali inapaswa ionyeshe moyo wa utu kwa kutoa kifuta machozi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao hasa baada ya kuwapo maelezo ya wazi kwamba watu walitafutwa na wakauawa kwenye kumbi, vyumbani, kwenye viambaza, kwenye magari nk. Aidha, nashauri majeruhi wote watibiwe kwa gharama za serikali. Kama pesa za risasi zipo, za matibabu haziwezi kukosekana. Hii si siasa, bali ni wajibu wa kiutu. Kwa kufanya hivyo, naamini serikali itakuwa imetuma ujumbe kwamba inaona, inasikia, na inajali.
Hakuna amani ya kweli katika taifa linaloshikilia viongozi wa kisiasa kwa mashitaka yenye sura ya kisiasa. Hakuna. Kama ishara ya kuanza ukurasa mpya, Rais Samia anaweza kutumia mamlaka yake ya kikatiba kufuta kesi zote za kisiasa, zikiwamo zile zinazowakabili viongozi na wanachama wa CHADEMA akiwamo Mwenyekiti Tundu Lissu, na Makamu wake, John Heche; na wengine wa vyama vingine vya ushindani. Hii haitakuwa ishara ya udhaifu, bali ni nguvu na busara ya uongozi. Kiongozi anayetaka amani ya kweli, sharti awe tayari kusamehe hata wale waliomkosea, kwani kusamehe ni hatua ya kwanza ya kuliponya taifa.
Watanzania wa leo, hasa vijana, wana kiu kubwa ya kusikilizwa. Pamoja na mambo ya utandawazi, mwamko wa vijana ni matokeo ya “shule za kata” zilizotoa fursa ya elimu kwa wengi. Wameelimika, wanajua haki zao, lakini pia wanaona pengo kati ya ndoto na uhalisia wa maisha yao. Ajira hazitoshi, gharama za maisha zimepanda, na sauti zao mara nyingi hazisikiki- wanazibwa midomo kwa kigezo kwamba kusema-sema ni kuhatarisha amani ya nchi.
Namshauri Rais Samia aanzishe Jukwaa la Taifa la Vijana, litakalokutanisha vijana kutoka kada zote kuanzia wanafunzi, wakulima, wajasiriamali, wanaharakati, na wasanii ili wazungumzie mustakabali wa nchi yao wakiwa wamoja. Naamini kuwa kuwasikiliza vijana ni kuwekeza kwenye amani ya kesho.
Rais Samia anaenda kulihutubia Bunge. Tumuombe na tumshauri atumie fursa hii kama Jukwaa la Ukweli na Upatanishi. Hotuba ya Bunge ndiyo, ama ya kuliokoa taifa, au kuliweka kwenye hali tete zaidi. Hili alijue mapema. Hatima ya Tanzania imo kwenye hotuba hiyo baada ya kutofanya hivyo kwenye uapisho.
Katika nyakati hizi za maumivu, taifa linahitaji kusikia sauti ya faraja kutoka juu kwa mfariji mkuu ambaye ni yeye Rais. Anaweza kutumia jukwaa la Bunge kusema serikali inatambua yaliyotokea, inasikitishwa, inachukua hatua kurekebisha, na itasimamia maridhiano ya kweli baada ya haki kutendeka. Wananchi wanasubiri aseme na atende.
Hotuba kama hiyo itakuwa ya kihistoria. Itazima au kupunguza hasira, itarudisha matumaini, na itaanzisha ukurasa mpya wa taifa lenye umoja. Huo ndio uadilifu ambao taifa linamtazamia Rais Samia auonyeshe. Asitoe hotuba ya kulaumu au kutisha maana kufanya hivyo kutaendelea kuwa ni kutonesha vidonda. Awe mnyenyekevu na atuisaidie kutuonyesha tunatoka vipi kwenye mtanziko huu wa kihistoria.
Nigusie Tume Huru ya Uchaguzi. Chanzo kimojawapo cha migogoro katika nchi nyingi ni ukosefu wa imani kwenye mchakato wa uchaguzi. Rais atafanikisha hili la uchaguzi endapo kama kutakuwapo Katiba mpya ili kuondokana na Tume ya aina hii ambayo imechukiwa hadi na jumuiya ya kimataifa.
Vilevile, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ipewe meno ya kisheria kufuatilia uvunjifu wa haki za binadamu na kuwalinda raia dhidi ya matumizi mabaya ya nguvu za dola. Tume ya sasa ambayo watendaji wake wakuu wanateuliwa na Rais, inadhaniwa haiwezi kuwa huru kufanya kazi za kuikosoa serikali inayoongozwa na aliyeiunda.
Watanzania wamechoka kuona makosa yakirudiwa bila wahusika kuchukuliwa hatua. Rais anaweza kuanzisha utamaduni wa uwajibikaji wa kweli ndani ya vyombo vya dola na utumishi wa umma. Kila ofisa atakayehusika na matumizi mabaya ya madaraka, rushwa au ukiukaji wa haki achukuliwe hatua bila kujali cheo chake. Hayo ndiyo yanayoliliwa na Watanzania wengi. Uwajibikaji ni silaha ya amani ya kudumu.
Rais Samia alianza kujijengea sifa ya uvumilivu, utulivu na busara. Nguzo hizi zinahitajika leo zaidi kuliko wakati mwingine wowote wa utawala wake. Taifa linamhitaji mama anayekemea, anayesamehe, anayelinda, anayesikiliza, na anayechukua hatua. Hili ndiyo dhima kubwa ya kihistoria aliyonayo sasa.
Amani ya kisiasa haina maana kama wananchi wanateseka kwa njaa na umasikini. Hata zijengwe shule, madaraja, barabara, hospitali na huduma zote za kila aina, kama wananchi hawana matumaini ya kula na kuishi, yote mengine ni kazi bure! Wananchi kama wananyimwa uhuru wa kuzungumza kwa uhuru, vifuani watajaza mengi ya chuki na matokeo yake ni mabaya.
Amani ni zao la haki. Haki ni zao la uadilifu na upendo. Kama taifa, tusikimbilie “maridhiano ya maneno” kabla hatujaweka wazi nini kilichotokea, nani aliumia, na nani alihusika. Sharti tujue mambo gani yametufikisha kwenye mauaji ya kinyama ya Oktoba 29. Ukweli utatusaidia kuondoka hapa tulipo. Hata kama jukumu la amani ni la kila mmoja wetu, dira yake sharti ionyeshwe na Rais mwenyewe kwanza.
Leo, Watanzania hawahitaji hotuba nyingi na ndefu. Wanahitaji kuona vitendo vya ujasiri. Wanadai haki, utu, na mwelekeo mpya wa taifa lao. Rais Samia akiongoza mchakato wa ukweli, maridhiano, na uponyaji, atakuwa ameandika ukurasa mpya wa historia ya Tanzania — ukurasa wa ujasiri, hekima na upendo. Kuna wakati wa kusema, na kuna wakati wa kutenda. Watanzania wanahitaji vitendo vya haki ili amani itamalaki. Wanataka waheshimiwe na wasikilizwe kama wadau muhimu kwa maendeleo ya taifa lao. Hawahitaji kufokewa kama wasio na thamani au maana. Nchi hii ni ya Watanzania wote.
Nimeyasema haya nikiwa raia mwema ninayeomba kwa Mungu nchi yetu iwe tulivu kwa misingi ya haki na amani. Kila anayeipenda Tanzania, na anayempenda Rais Samia, atafanya walau zaidi ya nilivyoshauri hapa.
Nimeyaandika nikiamini kwa dhati kuwa Woga Ndiyo Silaha Dhaifu Kuliko Silaha Zote. Nikiwa mwana-CCM niliyelelewa katika mikono ya waasisi ya utu na haki, naahidi kusimama kwenye ahadi ya “Nitasema Kweli Daima, Fitna Kwangu Mwiko”. Tunao wajibu halali wa kumshauri Rais yaliyo ya heri kwake na kwa taifa letu. Watawala wakipuuza kilio cha wananchi na kukumbatia hekaya za “machawa” na wanafiki, wataliua Taifa.
MUNGU IBARIKI TANZANIA
Manyerere J.N
0759488955
Novemba 10, [siku yangu ya kuzaliwa], 2025.


