📍Dodoma,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amefungua rasmi Bunge la 13 jijini Dodoma, akitoa dira mpya ya Maendeleo ya Taifa na vipaumbe atakavyoanza navyo kupitia sekta za uzalishaji, hususan kuongeza uwekezaji katika kilimo cha Umwagiliaji
Katika hotuba yake, Rais Dkt.Samia alisisitiza dhana ya “Kilimo ni Biashara, Mkulima ni Mwekezaji”, akibainisha kuwa Serikali inalenga kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo kutoka asilimia 4 ya sasa hadi kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.
*Malengo Makuu ya Serikali katika Kilimo cha Umwagiliaji.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa, Lengo si tu kuzalisha kwa wingi, bali kuongeza thamani ya mazao ili kuwanufaisha Watanzania wengi wanaofanya kazi katika sekta ya kilimo.

Ameongeza kuwa Serikali inalenga kuifanya nchi kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mahindi, mchele na mboga mboga barani Afrika na kwamba kupitia ruzuku ya pembejeo, mbolea na viuatilifu, wakulima watawezeshwa kuongeza tija na ubora wa mazao.
Kwa upande wa Kilimo cha Umwagiliaji amesema atahakikisha anaongeza uwezesha wa sekta ya hiyo kwa kuboresha na kujenga miundombinu ya Umwagiaji zaidi.
Alisema hatua hiyo itawezesha ongezeko la eneo la Umwagiliaji kutoka ekari milioni 3.4 za sasa hadi ekari milioni 5 na kwamba hatua hii itahusisha, Ujenzi wa mabwawa na skimu za Umwagiliaji, kuanzisha skimu mpya, ikiwemo katika bonde la Mto Rufiji na Kuanzisha vituo vya ukodishaji wa zana za kilimo ili kurahisisha upatikanaji wa teknolojia kwa wakulima nchini.
Dira ya Taifa
Kwa mujibu wa Rais, mapinduzi haya ya kilimo yataleta mageuzi makubwa katika uchumi wa Taifa, kuongeza ajira, na kuimarisha usalama wa chakula.
Hatua hizo pia zinatarajiwa kuimarisha nafasi ya Tanzania katika soko la kikanda na kimataifa.


