📌Vitongoji 936 vimefikiwa na huduma ya umeme Arusha
📌REA yaahidi kufikisha umeme kwa wakati ili kukuza uchumi wa wananchi
📍Arusha
Imeelezwa kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), amewezesha kuwasha umeme vijiji vyote 368 sawa na asilimia 100 na sasa utekelezaji unaendelea kwa kasi ya kupeleka huduma ya umeme kwenye vitongoji vyote ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo jijini Arusha.
Hayo yamebaibishwa leo Agosti 28, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, wakati wa ziara ya kutembelea utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, sambamba na kuzungumza na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA ambapo ameweza kushuhudia wananchi wakiunganishiwa huduma ya umeme Wilaya ya Arumeru, Kitongoji cha Kisongo Juu jijini humo.

Ameongeza kuwa, mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji unaendelea vizuri ambapo vitongoji 936 kati ya vitongoji 1,505 hadi sasa tayari vimeunganishwa na nishati ya umeme na kazi hiyo inaendelea kwa kasi ili kumaliza kwa wakati na wananchi waweze kunufaika na uwepo wa nishati ya umeme katika maeneo yao.
“Tumshukuru sana Mhe. Rais Samia kwa namna mbavyo anaendelea kuwezesha sisi REA kuweza kutekeleza miradi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji kwa kasi kubwa kama mnavyoiona katika mkoa huu wa Arusha na wananchi wengi wanaendelea kuunganishiwa umeme, ” Amesema Mhe. Balozi Kingu.
Vilevile, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika mkoa huu inayolenga kuwapatia huduma za uhakika za nishati ili kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi katika maeneo yote ya vijijini.

Katika hatua nyingine, Mhe. Balozi Kingu amehaidi kuwa, REA itaendelea kuwafikishia huduma ya umeme wananchi kwenye vitongoji na maeneo ya pembezoni ya miji ili kuwawezesha kuwa na umeme wa uhakika katika maeneo hayo na kuwezesha kukuza uchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kisongo Juu Adam William, amesema mradi huo wa umeme katika eneo hilo ni fursa kwao kuweza kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kusaga mahindi na mpunga kwa kutumia mashine ya umeme, kuchaji simu na fursa nyingine za kiuchumi zinazotokana na uwepo wa nishati ya umeme.

