📌Dkt. Biteko awaasa Watanzania kutogawanyika na kuendelea kuwa wamoja

📌 Awapongeza CCT kwa kuendelea kushirikiana

📌 Asema Serikali inathamini mchango wa CCT kwa maendeleo ya Taifa

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza upendo na amani miongoni mwa Watanzania sambamba na kufanya jitihada mbalimbali zitakazosaidia kuiletea nchi maendeleo.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Mei 25, 2025 jijini Mwanza aliposhiriki ibada ya maadhimisho ya Siku ya Jumuiya ya Kikristu Tanzania – CCT Kitaifa iliyofanyika KKKT Ushirika wa Ebenezer – Pasiansi.

“ Niwahakikishie kuwa milango ya Mhe. Rais Samia iko wazi, anataka Tanzania moja ya watu wanaopendana na kushirikiana ili kuifikisha nchi mbele kimaendeleo,” amesema Dkt. Biteko

Ametaja jitihada za Rais Samia kwa ajili ya kuleta amani, umoja na ushirikiano nchii kuwa ni pamoja na mikutano yake ya viongozi wa dini, kuruhusu mikutano ya hadhara pamoja na kuanzisha 4R’s yaani maridhiano, kuheshimiana, kujenga upya na kustahimiliana.

Kupitia ibada hiyo Dkt. Biteko amewataka Watanzania kutogawanyika na kubaki wamoja sambamba na kuendelea kuliombea Taifa ili liendelee kuwa na umoja na amani.

Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Watanzania kuheshimiana na kustahiliana kwa kuwa watu wote hawawezi kuwa na mawazo ya kufanana. Aidha, Serikali itamsikiliza kila mmoja ili kuwa na Taifa lenye upendo na amani huku akiwaasa wananchi kuheshimu sheria na katiba ya nchi.

Dkt. Biteko ameongeza kuwa watu wakosoane kwa heshima na kupanda mbegu njema kwa wengine kwa kuwa kwa mujibu wa vitabu vya imani kila analofanya mtu lina malipo yake. Huku akisisitiza watu kutenda haki.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali, itaendelea kushirikiana na CCT na madhehebu yote mengine ya dini kama ilivyowekwa msisitizo katika miongozo mbalimbali ya Serikali ikiwemo Sera ya Maendeleo ya Jamii ya mwaka 1996.

Ameongeza kuwa Serikali inathamini mchango wa CCT katika jamii na maendeleo ya Taifa kwa ujumla katika nyanja mbalimbali za afya, elimu, uchumi na malezi ya kiroho pamoja na kudumisha amani nchini.

Amebainisha baadhi ya maeneo ambayo yamefanyiwa kazi na CCT kuwa ni shughuli za umisheni na uinjilisti ili kukuza uongozi wa kiroho miongoni mwa vijana na jamii kwa mfano kupitia shughuli za UKWATA katika shule zote za sekondari nchini na USCF katika vyuo vikuu na vyuo vya kati 92 nchini.

“ Mmetengeneza ajira kwa vijana na jamii kwa mfano kutoka mwaka 2023 hadi 2025, mmetoa mafunzo ya walimu 200 wa sekondari na vyuo vya ufundi ili kuwasaidia wanafunzi katika ushauri wa kitaaluma na stadi za maisha. Pia katika kipindi hicho hicho, mmewajengea uwezo jumla ya vijana 45, 320 kuhusu masuala ya ajira na afya ya akili kupitia vyuo mbalimbali nchini,” amesema Dkt. Biteko.

Kuhusu uchumi na kilimo endelevu amesema kuanzia mwaka 2014 hadi 2025 wameanzisha na kusimamia zaidi ya vikundi vya kiuchumi yaani VICOBA 1, 840 nchi nzima vyenye mtaji wa zaidi ya shilingi bilioni 15 katika maeneo mbalimbali ikiwemo Bahi na Same.

Amezungumzia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa kuhamasisha Watanzania kushiriki katika mikutano na kugombea nafasi za uongozi.

Fauka ya hayo, Dkt. Biteko ameipongeza CCT na kuitaka kutoangalia tofauti za madhehebu yao bali kueneza injili nchini.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda amesema kuwa mamlaka zinatoka kwa Mungu hivyo ametoa wito kwa wananchi kuzitii mamlaka na wenye mamlaka wanatakiwa kutenda haki.

Pia, amewataka wananchi Mkoa wake kuishi kwa upendo, kushirikiana na kufanya kazi kwa bidii.

Awali, akihubiri katika ibada hiyo, Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Mt. Kilimanjaro na Makamu Mwenyekiti wa CCT, Dkt. Stanley Hotay amesema kuwa haki ni kitu ambacho mtu anastahili kuwa nacho na kuwa haki hizo zinalindwa na katiba ya nchi.

Amesema wakristu wanapaswa kujilinda kwa kuiombea nchi na mipaka yake hususan katika mikusanyiko ya watu.

Katika kipindi cha kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani amevishauri vyama vya siasa kutumia maneno ya staha katika majukwaa yao na wala wasikubali kushawishia kutenda uovu.

Kupitia ibada hiyo iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania – KKKT, Dkt. Alex Malasusa pamoja na maaskofu wa madhehebu ya kikristu 12 yanayounda CCT, maaskofu hao waliombea Taifa ili liendelee kuwa na amani.