Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameongoza maelfu ya Watanzania katika Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa yaliyofanyika leo tarehe 25 Julai, 2025 katika Uwanja wa Mnara wa Mashujaa, uliopo Mtumba Jijini Dodoma.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na viongozi wa kitaifa wakiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Katika kuonyesha heshima kwa mashujaa waliolitumikia taifa kwa ujasiri, Rais Samia ameweka mkuki na ngao katika mnara maalum, ikiwa ni ishara ya kutambua na kuthamini mchango wao kwa taifa tangu enzi za ukombozi hadi sasa.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo Rais Samia amesisitiza kuwa mashujaa wa Tanzania walijenga misingi ya uhuru, amani na mshikamano, hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kulinda misingi hiyo na kuwathamini waliopigania uhuru huo.

Amesema kuwa taifa lisiloenzi historia yake hujikuta likikosa mwelekeo wa maendeleo, hivyo vijana wa Tanzania wana wajibu wa kujifunza kutoka kwa mashujaa waliotangulia na kutumia maarifa yao katika kulinda rasilimali, amani na hadhi ya taifa kwa vizazi vijavyo.

Siku ya Mashujaa huadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Julai kama kumbukizi ya waliotoa maisha yao kwa ajili ya uhuru na maendeleo ya Taifa, ikiwa ni sehemu muhimu ya historia ya Tanzania na urithi wa kizalendo kwa vizazi vijavyo.