Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameongoza mamia ya waombolezaji katika kutoa heshima za mwisho kwa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Job Yustino Ndugai, katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

Rais Samia aliwasili majira ya asubuhi na kusaini Kitabu cha Maombolezo kabla ya kuungana na viongozi mbalimbali wa kitaifa, wabunge, ndugu, jamaa na marafiki katika ibada ya kuaga mwili wa kiongozi huyo mashuhuri. Baada ya ibada hiyo, alitoa heshima zake za mwisho kwa kugusa jeneza lenye mwili wa Hayati Ndugai, ishara ya heshima na kuenzi mchango wake mkubwa kwa taifa.

Katika tukio hilo lililohudhuriwa pia na viongozi wa Serikali, Bunge na vyombo vya ulinzi na usalama, Katibu wa Bunge, Baraka Leonard, alisoma wasifu wa marehemu na kuweka wazi sababu za kifo chake, akieleza kuwa Ndugai alifariki dunia Agosti 6, 2025, saa 9 alasiri, jijini Dodoma, kutokana na shinikizo la damu kushuka sana (septic shock) lililosababishwa na maambukizi makali ya mfumo wa hewa (severe pneumonia).