Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
RAIS wa awamu ya 6 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa kuanzisha mpango wa Bima ya Afya kwa wote hapa nchini kwa kuwa itawezesha wananchi kupata huduma bora za afya popote.
Pongezi hizo zimetolewa na Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Magharibi Dkt Emmanuel Lupilya alipokuwa akiongea na mwandishi wa gazeti hili juzi Ofisini kwake.
Amesema kuwa mswada huo uliopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 1, 2023, ulipitishwa rasmi kuwa sheria mwaka 2024 baada ya kusainiwa na Mheshimiwa Dkt Rais Samia Suluhu Hassan.
Amefafanua sheria hii itasaidia wananchi wote wa Tanzania Bara kupata huduma za matibabu kupitia mfumo wa Bima ya Afya kwa wote ambapo mwananchi atakuwa na uhuru wa kuchagua mtoa huduma yeyote wa Bima ya afya kumhudumia.

Dkt Lupilya ameeleza kuwa Bima hii ni muhimu sana kwa kuwa imelenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya mahali popote na kwa gharama nafuu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Ametaja baadhi ya faida za mpango huu kuwa ni kuwezesha kila mwananchi kupata huduma za afya bila kushindwa kumudu gharama kubwa za matibabu na kupunguza mzigo wa kifedha kwa familia pale wanapokumbana na changamoto.
Ameongeza faida nyingine kuwa ni kuimarisha huduma za afya nchini kwa kuongeza fedha zinazopatikana kupitia Bima na kusaidia makundi yenye kipato cha chini kupata huduma za afya bila kikwazo chochote cha kifedha.
‘Kwa niaba ya Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima, Dkt Baghayo Saqware na Naibu Kamishna Khadija Said, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha mpango huu wenye manufaa makubwa kwa wananchi’, ameeleza.
Dkt Lupilya ameeleza majukumu ya TIRA katika kuhakikisha mpango huu unaleta tija kuwa ni kusajili skimu za Bima ya Afya, kufuatilia ubora wa huduma za afya zinazotolewa katika vituo vyote na kutoa miongozo ya malipo kwa watoa huduma.
Mengine ni kuhakikisha Bima za Afya zinatoa kitita cha mafao ya msingi kwa mujibu wa sheria hii na.8 ya sheria ya Bima ya Afya kwa wote ya mwaka 2022 na kuhakikisha huduma za bima zinazotolewa zinaendana na viwango vya michango.
Aidha TIRA itatoa miongozo ya malipo, uendeshaji wenye ufanisi na tija, kutunza kanzidata ya vituo, kufanya ukaguzi wa skimu za bima, usajili wa wanachama, kuomba taarifa inayohitajika na kuhakikisha skimu ya bima ina ukwasi na akiba kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.