Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imesema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi la kuongeza nafasi za ajira 300 katika mamlaka hiyo.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala TRA, Moshi Kabengwe kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda imeeleza ajira hizo ni zile zilizokasimiwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26.

Kabengwe alieleza ajira hizo zitajazwa kwenye mchakato uliomalizika hivi karibuni na hivyo kufanya idadi ya watakaoajiriwa kuwa 1,896 badala ya 1,596 ya awali.

TRA ilimshukuru Rais Samia kwa kuridhia ombi hilo la kuongeza nafasi hizo za ajira.

Kabengwe alieleza Februari mwaka huu TRA ilitangaza nafasi za kazi 1,596 na ilipokea maombi ya kazi 135,027 kati yao 113,023 waliitwa kwenye usaili wa mchujo wa kuandika baada ya kukidhi vigezo na usaili huo ulifanyika Machi 29 na 30, mwaka huu.

Alisema wasailiwa waliofanikiwa kwenye usaili wa kuandika waliitwa kwenye usaili wa mahojiano uliofanyika Mei 12 hadi Mei 14, mwaka huu na wasailiwa 6,325 walifanya usaili huo.

Aidha, alieleza matokeo ya usaili huo yametolewa jana kupitia barua pepe zao walizotumia kuombea kazi.

“Wasailiwa 1,896 ambao wamefaulu na wameitwa kazini wanatakiwa kufika katika kumbi walizopangiwa Juni 2, 2025 wakiwa na nyaraka muhimu kama zilivyoainishwa kwenye barua pepe zao,” alisema kupitia taarifa hiyo.