Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wa chama hicho kuhakikisha mchakato wa kuwachuja wagombea unazingatia haki, maadili na maslahi ya chama pamoja na taifa kwa ujumla.
Akizungumza leo Mei 30,2029 wakati wa kufunga Mkutano Maalum wa CCM uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre (JKCC) jijini Dodoma, Rais Samia amesisitiza kuwa vikao vya uteuzi havipaswi kufanyika kwa misingi ya upendeleo au ushawishi wa watu binafsi.

“Vikao vinavyohusika na mchujo wa wagombea vina wajibu wa kufanya kazi kwa haki,tuwape nafasi wanaostahili na tuepuke kuwaingiza watu wenye mapungufu ya kiuongozi,” amesema Rais Samia.
Aidha, ametoa onyo kwa wanaojaribu kupenyeza wagombea kwa ushawishi wa muda mfupi au kupitia makundi ya maslahi binafsi, akieleza kuwa mwenendo huo unahatarisha uimara na maadili ya chama.
“Tukianza kupitisha watu kwa misingi ya kutafuta umaarufu wa muda mfupi au makundi maalum, tutaligeuza chama kuwa ‘Gwajimanist’. Tuwe waangalifu tusiiingize CCM katika mwelekeo huo; wale wa aina hiyo wabaki nje,” ameonya Rais Samia.

Kauli hiyo imeonekana kuwa ujumbe mahsusi wa kuendeleza mageuzi ya ndani ya chama, kwa lengo la kuhakikisha kuwa viongozi watakaochaguliwa ni wale wanaojikita katika utumishi wa kweli kwa wananchi na wanaojitambulisha kwa maadili mema pamoja na uwezo wa kiuongozi.
Mmoja wa wajumbe waliohudhuria mkutano huo Martha Jarome amezungumzia kauli hiyo ya Rais Samia na kueleza kuwa, “‘Kauli ya Mwenyekiti imetufumbua macho,tumezoea kuona watu wanaotumia fedha na ushawishi binafsi kupenya, lakini sasa kila mmoja wetu ataogopa kuvuruga taratibu,” amesema mjumbe huyo kutoka Kanda ya Ziwa.
Mjumbe mwingine kutoka Mkoa wa Kusini Unguja Mussa Hassan Idd ameongeza kuwa, “Ujumbe huu umetufikia vizuri,tunapaswa kuwachuja wagombea kwa kutumia vigezo vya uadilifu, sio kwa misingi ya kujuana au makundi ya kisiasa.”amesema na kuongeza;
“Mabadiliko haya ya kiuongozi ndani ya CCM ni lazima yaanze na sisi wenyewe, Tukiwa wakweli katika mchujo, chama kitaimarika zaidi na wananchi watatuamini zaidi,kwa ujumla kauli ya Rais Samia imeonekana kuwa sehemu ya dhamira ya kuendeleza mageuzi ya kweli ndani ya CCM, kwa lengo la kuimarisha nidhamu, uongozi bora, na utumishi wa umma wenye tija kwa wananchi, “Amesisitiza.




