Na Dotto Kwilasa,Jamhuri Media,Dodoma

Wakati zaidi ya watu milioni 83 duniani wakilazimika kuhama makazi yao kutokana na majanga ya asili, migogoro, na kuyumba kwa uchumi, Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuenzi mashujaa wa misaada ya kibinadamu ambapo safari hii kiongozi mkuu wa nchi amepewa heshima ya kipekee.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametunukiwa tuzo ya heshima ya juu kutokana na mchango wake mkubwa na wa kipekee katika kushughulikia maafa, kuongoza kwa hekima wakati wa majanga mbalimbali, na kusukuma mbele ajenda ya misaada ya kibinadamu nchini.

Tuzo hiyo imetolewa katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Watoa Huduma za Misaada ya Kibinadamu Duniani, yaliyofanyika leo kwenye ukumbi wa Mabeyo Complex jijini Dodoma, yakihudhuriwa na viongozi wa serikali, wawakilishi wa mashirika ya misaada ya kitaifa na kimataifa, na wananchi kutoka kada mbalimbali.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo kwa niaba ya Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, amesema kuwa tuzo hiyo ni uthibitisho wa uongozi thabiti wa Rais Samia katika kulinda maisha ya Watanzania hasa nyakati za dharura.

Mbali na Rais Samia, viongozi wengine waliotunukiwa tuzo ni Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wote kwa mchango wao katika kusimamia jitihada za serikali katika kutoa misaada na kuokoa maisha wakati wa majanga.

Mashirika na Taasisi zilizotambuliwa kwa mchango wao katika kutoa misaada ya kibinadamu ni pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, JWTZ, Wizara ya Ujenzi, World Food Programme (WFP), UNICEF, Save the Children, World Vision International, Caritas Tanzania, RAPID Tanzania, TRCS, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Uratibu wa Maafa.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika Yanayoshughulika na Maafa (DINGONET), Ruger John Kahwa, amesema maadhimisho haya yamekuja wakati dunia inakabiliwa na changamoto kubwa ya misaada ya kibinadamu.

Amesema kuwa zaidi ya watu milioni 13 duniani wanakumbwa na majanga kila mwaka, huku watoa misaada wakikumbwa na hatari kubwa kazini – ambapo kati ya Januari na Juni mwaka huu pekee, baadhi yao walipoteza maisha.

“Hali ni mbaya mahitaji ni makubwa lakini misaada ni midogo. Hata hivyo, watoa huduma wameendelea kujitolea kwa moyo wa kishujaa,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Waziri Lukuvi ameeleza kuwa serikali inaendelea kujizatiti katika kuimarisha mifumo ya dharura, ikiwemo kuanzisha “Situation Room” ya kitaifa kwa ajili ya kuratibu matukio ya maafa kwa wakati halisi. Alieleza kuwa serikali pia imewekeza kwenye miundombinu ya dharura, msaada wa chakula, huduma za afya na msaada wa kisaikolojia kwa waathirika wa majanga.

Ametoa mfano wa mafuriko ya mwaka 2024 katika maeneo ya Kilosa, Kilombero, Rufiji na Kibiti ambako juhudi za pamoja kati ya serikali na wadau ziliokoa maisha na kurejesha huduma muhimu.

Aidha, Lukuvi amehimiza watoa huduma kujiandaa kwa majanga kupitia mipango ya dharura, huku wananchi wakihimizwa kuhifadhi mazingira, kutumia nishati safi, na kushiriki katika kulinda utulivu wa taifa.

Pia amesema serikali imelipokea rasmi ombi la kuingiza siku hii ya watoa misaada kwenye kalenda ya kitaifa, na hatua zitachukuliwa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Maafa.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Ummy Nderiananga, amesisitiza kuwa “utu na huruma havina mipaka,” na kwamba kazi ya watoa misaada ni ya kishujaa inayopaswa kuheshimiwa na kuungwa mkono na kila Mtanzania.

“Maadhimisho haya si tu kumbukumbu kwa waliopoteza maisha yao wakiwa kazini, bali ni wito kwa kila mmoja wetu kushiriki katika kuijenga jamii yenye ustahimilivu na mshikamano wa kweli,” ameongeza.

Aidha Maadhimisho haya ni ya tatu kufanyika Tanzania yakianza mwaka 2022 jijini Dar es Salaam, kisha kurudi tena mwaka 2024 jijini humo, kabla ya kuhamia Dodoma mwaka huu ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Kuimarisha Utoaji wa Huduma za Kibinadamu na Ustahimilivu Dhidi ya Majanga.”