Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Julai 17, 2025, ameizindua rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, akibainisha kuwa inalenga kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati wa juu, kwa msingi wa maendeleo jumuishi, usawa wa kijinsia, mshikamano wa kitaifa na maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo uliyofanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, dini, vyama vya siasa, mabalozi na wadau wa maendeleo, Rais Samia amesema kuwa dira hiyo imebeba matarajio ya Watanzania kwa miongo ijayo, na hivyo utekelezaji wake lazima uwe wenye tija, unaopimika na unaozingatia uhalisia wa maisha ya watu.

“Hii ni dira ya matumaini,imelenga kutoa mwongozo wa namna bora ya kutumia rasilimali zetu kwa maendeleo ya watu lakini hatutaki ibaki kuwa nyaraka ya makabatini, bali chombo hai cha mabadiliko chanya,” amesema Rais Samia.

Aidha, ameiagiza Tume ya Taifa ya Mipango kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha wanatengeneza nyezo za kupima matokeo (performance measurement tools) zitakazosaidia kufuatilia utekelezaji wa dira hiyo kwa kila ngazi ya Serikali na jamii.

“Tunapaswa kuwa na mfumo madhubuti wa ufuatiliaji na tathmini,tunahitaji kujua tupo wapi, tunaelekea wapi, na ni nini kinatufanya tusonge au tusisonge,” amesisitiza.

Akizungumzia Umuhimu na Maudhui ya Dira ya 2050Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema Dira hiyo imeandaliwa kwa kushirikisha makundi mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, ikiwa ni pamoja na wadau wa maendeleo, sekta binafsi, wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Prof. Kitila amesema kuwa dira hiyo imeandikwa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza, na iliridhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Juni mwaka huu.

“Hii ni dira shirikishi, inayolenga kuweka misingi ya maendeleo endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho. Imelenga pia kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi wa ushindani na viwanda unaotoa ajira na kukuza ubunifu,” ameeleza.

Aidha ameitaja misingi Mikuu ya Dira ya 2050 kuwa ni pamoja na Demokrasia, Haki na Uhuru,Utu, Amani na Umoja wa Kitaifa,Utajiri na Matumizi Endelevu ya Rasilimali Asilia,Utamaduni na Maadili ya Kitaifa na Uchumi wa Kisasa unaojumuisha wote.

Amefafanua kuwa Dira hiyo imeweka vipaumbele kwenye sekta za elimu, afya, teknolojia, kilimo cha kisasa, mabadiliko ya tabianchi, miundombinu na ushirikishwaji wa wanawake na vijana.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa dira hiyo ni muhimu kwani hakuna taifa linalopata maendeleo kwa kubahatisha.

“Maendeleo hayaji kwa bahati mbaya. Yanahitaji mipango madhubuti. Dira hii ni mwanzo mzuri kuelekea miaka ijayo yenye matumaini,” amesema Dkt. Mpango.

Naye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amepongeza uandaaji wa dira hiyo akisema inajikita kwenye mahitaji ya watu, hasa kupitia uwekezaji katika rasilimali watu, usimamizi wa mazingira na usawa wa kijinsia.

Kwa upande wa sekta binafsi, mfanyabiashara na mwekezaji maarufu Rostam Azizi, amesema kuwa dira hiyo ni nyenzo sahihi ya kujenga taifa lenye ushindani wa kimataifa. Ametoa wito kwa Serikali kuhakikisha utekelezaji wake unakwenda sambamba na hali halisi ya jamii.

“Ni vizuri kupanga, lakini ni bora zaidi kutekeleza kwa ufanisi. Dira hii ni nafasi ya kuwalea vijana wetu kwa ubunifu, ujuzi na maadili ya kizalendo,” amesema Rostam.

Ameongeza kuwa sekta binafsi itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha dira hiyo inatekelezwa kikamilifu kwa manufaa ya vizazi vijavyo.