Na Kulwa Karedia, JamhuriMedia, Bahi

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amesema serikali imejipanga kufikisha maji kutoka Ziwa Victoria hadi Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma.

Amesema hatua hiyo itasaidia kumaliza tatizo la maji yenye chumvi linalowakabili wananchi wa eneo hilo.

Rais Samia amesema hayo leo Septemba 9 wakati akiomba kura kwa wananchi wa Bahi, ikiwa ni majibu ya ombi la mgombea ubunge wa jimbo hilo, Kenneth Nollo, ambaye aliiomba serikali kulipa kipaumbele suala hilo kutokana na umuhimu wake kwa afya, maisha na uchumi wa wananchi wa eneo hilo.

“Hapa kwetu wananchi wanatumia maji ya chumvi nyingi. Ombi letu kubwa kwa serikali ni kuunganishwa na chanzo cha maji safi kutoka Ziwa Victoria, tunaomba sana tuangaliwe kwa jicho la huruma. Hapa tulipo i ni lango kuu la kuingilia Jiji la Dodoma, hivyo maji safi na salama yanahitajika,” amesema.

Akijibu hoja hizo,,Rais Samia amesema serikali tayari inaendelea na miradi ya maji katika vijiji 56.

Amesema lengo kubwa la Serikali na endapo akichaguliwa ni kuhakikisha maji ya Ziwa Victoria yanawafikia wakazi wa eneo hilo kwa matumizi ya nyumbani na shughuli za kilimo cha umwagiliaji.

“Hapa lisipite maji ya Ziwa Victoria yaachiwe Hilo ndiyo kusudio letu. Sio kwa ajili ya maji ya kunywa tu, bali pia kwa kilimo,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema nchi nzima inahitaji maji, na serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji kwa kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hiyo muhimu kwa maendeleo ya jamii.

“Tunapokwenda mbele, dhamira yetu ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji. Tanzania inahitaji maji, na sisi tumedhamiria kuyafikisha kila kona,” aliongeza.

Mbali na sekta ya maji,Rais Samia amesema miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa wilayani Bahi, ikiwemo elimu, miundombinu, na reli ya kisasa (SGR).

Amesema kituo cha pili na cha tatu cha SGR kitajengwa pamoja na bandari kavu, hatua itakayofungua fursa za kiuchumi wilayani humo.

“SGR inaenda kubadilisha hali ya Bahi. Inafungua fursa na kuvutia uwekezaji. Tunatambua kuna madai ya fidia, tunayafanyia uhakiki na malipo yatafanyika,” alieleza.

Kuhusu barabara,amesema madaraja tisa tayari yamejengwa na barabara nyingi za changarawe zinapitika, huku akiweka wazi kuwa barabara ya Mwanachungu–Bahi kuelekea SGR itajengwa kwa awamu mbili, kutokana na umuhimu wake.

“Wito wangu ni kila mtu ajitokeze kupiga kura. Tufanye kazi hii ya kuchagua viongozi, tusibaki majumbani. Tukifanya hivyo, ahadi zote tutazitekeleza kwa vitendo.”amesema