Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali imejipanga kuhakikisha hakuna mtoto anayefika darasa la tatu bila kuwa na uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu, akisisitiza kuwa huo ndio msingi wa elimu bora na maendeleo ya taifa.

Rais Samia aliyasema hayo leo Januari 29, 2026 wakati wa akizindua Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali na wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili, mpango unaolenga kuimarisha msingi wa elimu ya awali nchini.

Amesema mpango huo ni utekelezaji wa ahadi alizotoa katika siku 100 wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, na unalenga kuweka msingi imara wa elimu kwa watoto ili waweze kukabiliana na masomo yao ngazi kwa ngazi katika mazingira ya mabadiliko ya sayansi, teknolojia na mahitaji ya dunia ya sasa.

“Mkakati huu ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayosisitiza maendeleo ya rasilimali watu, taifa linaloongozwa na maarifa na uadilifu, pamoja na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023, inayolenga kuandaa kizazi chenye maarifa, stadi, maadili na uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa.

“Tunaweza kujenga miundombinu mizuri na kuendeleza teknolojia, lakini tusipoimarisha msingi wa elimu ya awali kwa watoto wetu, tutakuwa tunajenga juu ya msingi dhaifu,” amesema Rais Samia, akibainisha kuwa changamoto za ubora wa elimu katika ngazi za juu zinatokana na udhaifu katika hatua za awali za ujifunzaji.

Rais Samia pia amefafanua kuwa maboresho ya mitaala ya elimu ya lazima kuwa ya miaka kumi yanalenga kuhakikisha watoto wanapata maandalizi sahihi tangu awali, ambapo mpango huo unatekeleza maazimio ya kikanda na kimataifa, ikiwemo Azimio la Umoja wa Afrika la mwaka 2024 pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, hususan lengo namba nne kuhusu elimu bora kwa wote.

Akisisitiza umuhimu wa ujifunzaji shirikishi, Rais Samia amepongeza matumizi ya nyenzo za kufundishia zinazotokana na mazingira ya ndani, kama mchanga, mbao, pumba za mpunga na vifaa rahisi, ambavyo vinamwezesha mtoto kujifunza kwa vitendo na kuelewa haraka.

Amesema serikali imejipanga kuhakikisha hakuna mtoto anayefika darasa la tatu bila kuwa na uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu, wakiwemo watoto wenye mahitaji maalum.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ameeleza mafanikio ya serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu, akisema idadi ya madarasa ya shule za msingi na sekondari imeongezeka kwa kiasi kikubwa tangu mwaka 2021, hatua ambayo imechangia kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kuboresha mazingira ya ujifunzaji.

Kuhusu rasilimali watu, Rais Samia amesema serikali imetekeleza ahadi yake ya kuajiri walimu 7,000 ndani ya siku 100 za mwanzo wa uongozi wake, ambapo walimu 6,044 tayari wameajiriwa na kupangiwa vituo vya kazi, huku mchakato wa ajira kwa nafasi zilizosalia.

“Maboresho ya miundombinu na ajira pekee hayatoshi bila kusimamia ubora wa ufundishaji, hivyo nitoe wito kwa wakaguzi wa elimu kuhakikisha mpango wa KKK unatekelezwa ipasavyo shuleni, tathmini za mara kwa mara zifanyike ili kubaini mapema watoto wenye changamoto na kuwapatia msaada kwa wakati,” amesema Rais Samia.

Amewataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa serikali katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora kuanzia hatua za awali, akisisitiza kuwa kuwekeza katika stadi za awali za watoto si hiari, bali ni wajibu wa pamoja kwa maendeleo ya taifa.

Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema mpango mkakati huo umejengwa katika misingi mikuu mitano, ikiwemo kuimarisha mbinu za ufundishaji kupitia mafunzo endelevu kwa walimu wa elimu ya awali, darasa la kwanza na la pili, maendeleo endelevu ya walimu hususan katika uandaaji wa vifaa vya kufundishia, pamoja na upatikanaji wa nyenzo za kujifunzia zinazopatikana kirahisi katika mazingira ya ndani kama vifuniko vya chupa na vifaa vingine rahisi.

Ameongeza kuwa mpango huo pia unajumuisha upimaji na tathmini za mara kwa mara ili kufuatilia maendeleo ya watoto kitaaluma.

“Utekelezaji wa mpango huu, utakaochukua kipindi cha miaka mitano kuanzia 2025 hadi 2030, utaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu, TAMISEMI, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla, na serikali itakuwa ikitoa mrejesho wa utekelezaji kila mwaka… lengo kuu ni kuhakikisha Watanzania wanaona matokeo halisi ya ahadi ya Rais Samia kwa kuwajengea watoto msingi imara wa kusoma, kuandika na kuhesabu tangu hatua za awali za elimu,” amesema Profesa Mkenda.

Awali, akitoa taarifa fupi kuhusu Mpango mkakati huo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Profesa Said Mohamed, amesema kuwa uimarishaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) katika elimu ya awali na madarasa ya kwanza ni msingi muhimu wa mafanikio ya elimu kwa mtoto.

Amesema kuwa umri wa miaka mitano hadi saba ni kipindi nyeti katika ukuaji wa mtoto, kwani mtoto asipopata maarifa ya KKK kwa wakati, huathirika kiakili, kimwili, kijamii na kihisia katika hatua zote za ujifunzaji.

“Baraza la Mitihani limekuwa likiendesha upimaji wa stadi za KKK kwa njia ya sampuli tangu mwaka 2015 katika halmashauri zote nchini, ambapo wanafunzi wa darasa la pili walipimwa sambamba na ukusanyaji wa taarifa kuhusu mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

Matokeo ya upimaji huo kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi 2023 yanaonyesha kuwa kati ya asilimia 67 hadi 87 ya wanafunzi walikuwa na umahiri wa jumla wa stadi za KKK, huku stadi ya kusoma na kuandika ikionesha matokeo bora zaidi ikilinganishwa na kuhesabu,” amesema Profesa Mohamed.

Hata hivyo, amesema kuwa upimaji huo ulibaini changamoto mbalimbali ikiwemo wanafunzi kushindwa kusoma maneno yenye silabi changamano, kusoma kwa kasi na ufasaha, pamoja na changamoto za matamshi zinazochangiwa na athari za lugha mama.

“Changamoto nyingine zilihusisha uandishi wa maneno yenye miundo tata, matumizi sahihi ya herufi kubwa na ndogo, pamoja na ugumu wa kufanya mahesabu yanayohitaji kubeba au kukopa,” amebainisha.

Kutokana na changamoto hizo, Profesa Mohamed amesema hatua zimechukuliwa ikiwemo kutoa mafunzo kwa walimu wa elimu ya awali na msingi, maafisa elimu na wadhibiti ubora wa shule nchi nzima.

Amefafanua kuwa NECTA imeendesha mafunzo kwa walimu 43,101 katika kipindi cha miaka mitatu, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kisayansi unaolenga kuhakikisha mwanafunzi anamudu stadi za KKK ifikapo darasa la tatu na kuendelea kujifunza kwa ufanisi.