Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi katika mikoa ya Simiyu na Mwanza kuanzia tarehe 15 hadi 21 Juni mwaka huu ambao atakagua miradi ya maendeleo, kabla ya kushiriki Tamasha la Utamaduni la Bulabo litakalofanyika mkoani Mwanza.

Akizungumza jijini Dodoma leo Juni 11, 2025 kwenye Ofisi mpya za wizara hiyo zilizopo Mji wa Serikali-Mtumba,Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa, amesema Rais Samia ataanza ziara hiyo kwa kutembelea wilaya za Meatu, Itilima, Bariadi na Maswa katika mkoa wa Simiyu, kisha kuelekea Mwanza kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la Kigongo–Busisi, mojawapo ya madaraja makubwa zaidi barani Afrika.

“Tarehe 21 Juni, Rais atashiriki Tamasha la Utamaduni la Bulabo, ambalo linatarajiwa kuwakutanisha wananchi wa kada mbalimbali kusherehekea na kudumisha urithi wa kitamaduni wa taifa letu,” amesema Msigwa na kuongeza kuwa tamasha hilo linaratibiwa na Wizara ya Habari.

Katika hatua nyingine, Rais Samia pia anatarajiwa kufanya ziara nje ya nchi ambapo atakuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Msumbiji, kama ishara ya kuimarisha uhusiano wa kihistoria na kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.

“Ziara hiyo ni sehemu ya mahusiano ya muda mrefu yaliyowekwa na waasisi wa mataifa yetu,vilevile, Rais atatembelea Visiwa vya Comoro tarehe 6 Julai, kushiriki maadhimisho ya Uhuru wa taifa hilo,” amebainisha Msigwa.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu huyo amesema kuwa kesho, tarehe 12 Juni mwaka huu,Wizara ya Fedha na Mipango itawasilisha Bungeni Bajeti Kuu ya Serikali pamoja na Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2025 na hivyo kutoa wito kwa watanzania kufuatilia kwa ukaribu tukio hilo.

“Bajeti hii ni ya mwisho katika Awamu ya Sita na inalenga kumalizia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025.hii pia ni bajeti ya uchaguzi, hivyo ni muhimu kwa Watanzania wote kuielewa na kujivunia hatua tulizofikia,” amesema.

Msigwa amesisitiza kuwa Rais Samia amewataka waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla kufanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu. “Rais amenituma niwaambie: Fanyeni kazi zenu vizuri na kwa Uhuru,Rais anaithamini sana taaluma ya habari, ” anasisitiza Msigwa.