Na Mwandishi Wetu, JamhuriMddia, Dodoma

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan anatarajia kuanza kampeni zake mkoani Singida Septamba 9, mwaka huu.

Kuanza kampeni zake mkoani Singida kumekuja baada ya kumaliza kampeni hizo katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe na Njombe ambako kote alikopita amepata mapokezi makubwa na kunadi Ilani ya CCM ya mwaka 2025-30.

Katika mikutano yake yote, Rais Samia amekuwa akielezea mikakati mbalimbali ambayo endapo akichaguliwa tena ataitekeleza.

Moja ya mikakati hiyo, akiwa mkoani Mbeya aliwaahidi wananchi kuwa wakikichagua chake atahakikisha anaimarisha na kuboresha Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), miundombuni ya barabara pamoja na kujenga bandari kavu katika eneo la Katenjele Mpemba mkoani Songwe ili kuhakikisha wakulima wanasafirisha mazao yao kwa wakati.

Mikoa ya nyanda za juu kusini ni maarufu kwa kilimo cha mazao ya parachichi, pareto na kahawa ambayo huliingizia taifa fedha nyingi za kigeni.

Akiwa mkoani Singida anatarajia kufanya mikutano mikubwa kwa sababu mkoa huo una wafuasi wengi wa CCM ambao wana shauku ya kusikia ahadi mbalimbali za Rais Samia, ikiwamo ya kuwaomba kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.