Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa mradi mkubwa wa uchimbaji wa madini ya Uranium yaliyopo katika Kijiji cha Mkuju wilayani Namtumbo Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahamed Abbas Ahamed alisema kuwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwasili Julai 30, mwaka huu katika uwanja wa Ndege wa mjini Songea na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali kisha ataanza safari ya kuelekea wilayani Namtumbo.
Mkuu wa Mkoa huyo Kanali Abbas alisema kuwa akiwa wilayani Namtumbo Rais Dk Samia Suluhu Hassan atazindua mradi mkubwa wa Madini ya Uranium ambayo ni mradi mkubwa unaosimamaiwa na kampuni ya Mantra na baadae ataelekea Kijiji cha Likuyu ambako ataongea na wananchi kwenye mkutano wa adhara.
Alisema kuwa mradi huo wa madini ya Uranium unaotarajiwa kuzinduliwa na Rais Dk Samia ni kati ya miradi mkubwa ya kimkakati nchini na unaotarajiwa kuleta Mapinduzi makubwa ya kiuchumi Kwa wananchi wa Wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma na Tanzania kwa ujumla.
” Ndugu waandishi wa Habari mradi huu unamchango mkubwa katika kukuza Pato la Taifa kupitia Mapato ya Kodi, ajira Kwa wananchi na kuchochea Maendeleo ya miundombinu katika maeneo jirani ” alisema mkuu huyo wa Mkoa.
Hata hivyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi maeneo yale ambayo Rais Dk Samia Suluhu Hassan atakapopita na hasa kwenye eneo la tukio.
