Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na Rais wa Jamhuri ya Burundi, Meja Jenerali Mstaafu Evariste Ndayishimiye, leo wamezindua rasmi Kiwanda cha Mbolea cha ITRACOM kilichopo Nala, Jijini Dodoma Kiwanda ambacho ni cha mwekezaji wa Burundi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo June 28,2025 Jijini Dodoma Rais Samia amewataka viongozi wa kiwanda hicho kuimarisha mfumo wa usambazaji wa mbolea ili kuwafikia wakulima waliopo maeneo ya vijijini kwa bei nafuu, huku akisisitiza umuhimu wa utoaji wa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa ajili ya kuongeza tija na kulinda afya ya udongo.

“Natoa rai kwa uongozi wa ITRACOM kuhakikisha kuwa mbolea inawafikia wakulima wote hususan walioko vijijini kwa bei nafuu na kwa wakati. Lakini zaidi ya hapo, elimu ya matumizi bora ya mbolea hizi ni lazima itolewe, ili wakulima watumie kulingana na aina ya zao na ardhi,” amesisitiza Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesema uwekezaji huo ni mfano bora wa ushirikiano wa kanda ya Afrika Mashariki, unaolenga kuongeza uzalishaji, ajira kwa vijana na wanawake, na kuimarisha usalama wa chakula katika ukanda huo.

Amesema kiwanda hicho kinatarajiwa kuwa sehemu ya mkakati wa taifa wa mapinduzi ya kilimo kupitia pembejeo bora.

Kwa upande wake, Rais wa Burundi, Meja Jenerali Mstaafu Evariste Ndayishimiye, ameuelezea uzinduzi huo kama hatua muhimu ya kihistoria inayodhihirisha mageuzi makubwa katika uhusiano wa mataifa hayo mawili.

“Zamani raia wetu walikuja Tanzania kama wakimbizi, leo tunakuja kama wawekezaji,huu ni uthibitisho wa mshikamano wa kweli kati ya Burundi na Tanzania,uwekezaji huu hautaboresha tu kilimo, bali utajenga undugu na uchumi wa kikanda,” amesema Rais Ndayishimiye.

Naye Waziri wa Kilimo wa Tanzania, Hussein Bashe, ameeleza kuwa serikali ya awamu ya sita imeweka msukumo mkubwa katika maendeleo ya kilimo kupitia mpango wa ruzuku ya mbolea, ujenzi wa mabwawa, na uhamasishaji wa matumizi ya pembejeo bora.

Amesema zaidi ya shilingi bilioni 500 zimetumika kwa wakulima wa korosho pekee, huku zaidi ya milioni 700 zikitengwa kwa ruzuku ya mbolea kwa mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa ITRACOM, Nduwimana Nazaire, amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha mbolea hadi tani milioni moja kwa mwaka na tayari kimetoa ajira zaidi ya 1,800 za moja kwa moja pamoja na zaidi ya 3,000 zisizo za moja kwa moja.

“Tulianza mradi huu mwaka 2020, sasa umefikia hatua ya kuzalisha aina 14 tofauti za mbolea, zenye uwezo wa kuboresha mazao kwa mazingira tofauti ya kilimo Afrika Mashariki,ushirikiano wa Tanzania na Burundi ndio uliofanya ndoto hii kuwa halisi,” amesema Nazaire.

Kiwanda cha ITRACOM kinatajwa kuwa miongoni mwa viwanda vikubwa zaidi vya mbolea katika kanda ya Afrika Mashariki, kikilenga kutosheleza soko la ndani la Tanzania pamoja na mataifa jirani kama Kenya, DR Congo, Rwanda, na Burundi yenyewe.