* Azindua Kiwanda cha Majaribio cha Uchenjuaji Urani Namtumbo- Ruvuma

*Mradi kuzalisha tani laki 3 za Urani kwa mwaka

*Serikali inamiliki hisa asilimia 20 ya mradi

 Namtumbo – Ruvuma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa Mradi wa Uchimbaji na Uchakataji Madini ya Urani uliopo katika Eneo la Mto Mkuju, Wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma, ni hatua ya kimkakati itakayoiweka Tanzania katika ramani ya dunia kwa kuifanya kuwa miongoni mwa mataifa kumi yanayoongoza kwa uzalishaji wa madini hayo muhimu duniani.

Amesema hayo leo Julai 30, 2025, wakati akizungumza na wananchi katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Kiwanda cha Majaribio cha kuchenjua madini ya urani kilichopo Mto Mkuju, hatua inayoashiria mwanzo wa safari ya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji na uchakataji wa urani barani Afrika.

Rais Samia amesema kuwa, hatua hiyo ni ssehemu ya mkakati wa Tanzania kufikia uchumi wa kati kupitia matumizi bora ya rasilimali asilia, ikiwemo madini ya urani ambayo yana thamani kubwa kimataifa.

“Ni siku ya historia kwa nchi yetu, kwani Tanzania inaanza rasmi safari ya kuwa mzalishaji mkubwa wa madini ya urani duniani kwa mara ya kwanza katika kiwango hiki. Urani ni moja ya madini mkakati tuliyobarikiwa kuwa nayo, na upatikanaji wake utachangia katika kuzalisha nishati salama na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika sekta ya madini duniani.” Amesema Rais Dkt. Samia.

Rais Dkt. Samia amesema kuwa, kwa hatua hiyo, Tanzania inajiweka kuwa kitovu cha utafiti na uchakataji wa urani duniani na Afrika, hatua itakayofungua fursa mpya za kiteknolojia, kitaaluma na kiuwekezaji nchini na kuifanya Tanzania kuingia katika ramani ya dunia kuwa miongoni mwa nchi 10 zinazozalisha urani duniani, na hivyo kuvutia uwekezaji wa kimataifa katika sekta ya madini mkakati.

Ameongeza kuwa, Sekta ya Madini ni miongoni mwa vipaumbele vya Dira ya Taifa ya 2050, kwq kwamba kupitia sekta hiyo, Tanzania inalenga kukuza uchumi wa viwanda unaotumia teknolojia ya hali ya juu pamoja na usimamizi bora wa rasilimali madini.

Manufaa ya Mradi huu ni pamoja na Gawio la Serikali ambapo Asilimia 20 ya hisa zinazomilikiwa na Serikali zinatarajiwa kuleta takribani dola milioni 40 kwa mwaka, fedha zitakazosaidia miradi ya maendeleo. Manufaa mengine ni pamoja na ajira kwa Watanzania, utafiti, mapato na mrabaha

Aidha, Rais Samia ameelekeza Mradi huo kuwa shirikishi kwa jamii kupitia miradi ya kijamii (CSR) ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara sambamba na kuzingatia taratibu za ulindaji mazingira ili kulinda mfumo wa ikolojia wa eneo la Mto Mkuju.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amemshukuru Rais Samia kwa kuipa sekta ya madini kipaumbele, jambo lililopelekea kuanzishwa kwa miradi mikubwa ikiwemo huo wa Mkuju.

Amesema mradi huo ni mkubwa zaidi Afrika Mashariki na Kati, na Tanzania sasa inakuwa miongoni mwa nchi tano pekee barani Afrika zenye miradi mikubwa ya uzalishaji urani wa aina hiyo na kwamba hatua hiyo ni matokeo ya mazingira rafiki kwa uwekezaji yaliyoandaliwa na Serikali chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Aidha, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa Sheria ya Madini inawataka wamiliki wa leseni kuhakikisha jamii zinazozunguka miradi zinanufaika moja kwa moja kupitia miradi ya kijamii (CSR).

Naye, Rais wa Kampuni ya Uranium One, Pavel Larionov, amesema kuwa mradi huo utakuwa ukizalisha takribani tani 300,000 za urani kila mwaka, na unatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa madini hayo kimataifa huku Tanzania ikipata mapato na nafasi za ajira kwa wingi.