Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan wiki iliyopita ameweka historia nyingine na kuanza safari ya historia ya kudumu kuelekea kupatikana kwa Rais wa Tanzania mwanamke aliyechaguliwa. Agosti 9, 2025 amechukua fomu ya kugombea urais kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) akiwa na Mgombea Mwenza, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi (wengine waliochukua fomu soma habari kuu).

Sitanii, leo sitarejea historia ya Rais Samia jinsi alivyoingia kwenye siasa na kufikia hapa alipofika. Nitagusia kwa uchache historia yake kuanzia Machi 17, 2021. Tarehe hii ni tarehe ya kipekee kwa Tanzania. Ni tarehe ambayo katika historia ya nchi yetu Rais aliyeko madarakani, Dk. John Pombe Joseph Mafufuli alifariki dunia. Mungu amlaze mahala pema peponi.

Nimeigusia tarehe hii, kwa maana huwezi kutenganisha safari ya Rais Samia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kumgusia Dk. Magufuli. Mwaka 2015, hayati Rais Magufuli alimteua Dk. Samia kuwa Mgombea Mweza katika uchaguzi uliokuwa na ushindani wa kweli. Ushindani ulikuwa mkubwa ndani ya chama, kwani walijitokeza wagombea 42 na nje ya chama baada ya kuundwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) uliotikisa nchi na kutoa mtihani halisi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Nasema mtihani halisi, kwa maana kwamba mitihani mingine iliyopita ukiwamo wa mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010 ilikuwa mitihani ya majaribio. Nani asiyekumbuka moto aliouwasha Edward Ngoyai Lowassa? Nani asiyekumbuka kuwa Lowassa alipata kura nyingi kuliko mgombea yeyote wa upinzani aliyepata kutokea hapa nchini, wakiwamo Agustino Lyatonga Mrema (1995), Profesa Ibrahim Lipumba (2000), Freeman Mbowe (2005) na Dk. Wilbroad Slaa (2010).

Dk. Magufuli na Rais Samia (wakati huo 2015) walilishinda jaribio hili la kuifanya CCM kuwa chama cha upinzani kama UNIP (Zambia – 1991), MCP (Malawi – 1994), Labour Party (Mauritius – 1982), BNP (Lesotho – 1993), AREMA (Madagascar – 1993), SPPF (Seychelles – 2016), KANU (Kenya – 2002) na vingine vingi.

Sitanii, swali ni je, kwa nini vyama hivyo vilishindwa? Jibu lipo. Havikuwatumikia wananchi. Swali mbadala linakuja, nalo ni je, kwa nini CCM imeendelea kuwapo madarakani? Jibu ni inawatumikia wananchi. Nafahamu kwa kulisema hili, wapo wanaokereka. Tumejazana upepo na kila mara tunaambiana eti nchi ya Rwanda imepiga hatua kubwa katika maendeleo.

Nataka kutoa indhari. Tusilinganishe tembo na sungura. Tanzania ni nchi yenye eneo kubwa zaidi ya nchi nne za Afrika Mashariki zikiunganishwa yaani Kenya (582,646 sq km), Uganda (241,038 sq km), Rwanda (26,338 sq km) na Burundi (27,834 sq km). Eeneo la nchi hizi nne ukiliunganisha ni kilomita za mraba 877,856. Jumlisha mwenyewe uone. Wakati tangu enzi tulitambua ukubwa wa Tanzania kuwa ni kilomita za mraba 947,068, taarifa mpya ya Benki ya Dunia inaonyesha kuwa ukubwa wa Tanzania ni kilomita za mraba 947,300. Ni nchi ya 13 kwa ukubwa barani Afrika.

Sitanii, nimeeleza indhari hii kwa nia ya kuwaonyesha na kuweka mlinganyo katika dhana ya maendeleo. Mkoa mkubwa Tanzania ni Tabora ambao una eneo lenye kilomita za mraba 76,151. Ukubwa wa mkoa huu, narudia ukubwa wa Mkoa wa Tabora ni sawa na nchi 2.89 za Rwanda. Kimsingi kwa eneo la Rwanda Tabora ilistahili kuwa nchi tatu. Hapo hujagusa mikoa 30 ya Tanzania iliyosalia. Kwa eneo la nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kuwa kilomita za mraba 877,856 na Tanzania kuwa 947,300, ni wazi eneo la Tanzania ni kubwa zaidi kwa kilomita za mraba 69,444 kwa nchi hizo zikiunganishwa.

Baada ya usuli huo, fikiria Rwanda wangejenga barabara moja ya lami kutoka Dar es Salaam hadi Bukoba kilomita 1,415 au Dar es Salaam – Kigoma kilomita 1,245 nchi ya Rwanda ingejenga barabara kiasi gani? Nakuhakikishia ingejenga hadi uchochoroni. Kwa mantiki hiyo niseme yeyote anayezungumza juu ya CCM kuleta maendeleo hadi vijijini alifikirie hilo la ukubwa wa eneo la nchi, kisha aendelee na mjadala.

Nikirejea kwa Rais Samia, niseme tu kuwa wiki iliyopita ameandika historia itakayoendelea kudumu kwa miaka mingi. Amekuwa mwanamke wa kwanza kugombea urais kupitia chama tawala. Nafahamu utasema waliwahi kugombea akina Anna Senkolo na wengine kupitia upinzani, hili haliondoi ukweli kuwa hawa waligombea kama washereheshaji, hawakuwa washindani.

CCM kwa misingi na mizizi iliyojijengea mijini na vijijini, nakuwa mkweli kwa nafsi yangu, kwa sasa wagombea ubunge wanaweza kuwa na hofu ya kushindwa maeneo ya mijini, ila mgombea urais wa CCM kuna kila ishara kuwa ndiye anakuwa rais ajaye. Na CCM ikiendelea na utamaduni wa kusikiliza kero za wananchi ikazifanyia kazi, naiona ikiendelea kuwa madarakani kwa muda mrefu kama CPC ya China. Inawezekana msomaji mmoja au wawili wasilipende hili ila huo ndiyo ukweli wenyewe.

Maono ya Rais Samia tumeyashuhudia kwa hii miaka minne. Ametekeleza miradi mikubwa iliyoanzishwa na mtangulizi wake kwa kiwango ambacho wengi walisubiri ashindwe wamsute. Mradi kama Bwawa la Mwalimu Nyerere linalozalisha umeme megawati 2,115, kusimamia ujenzi wa makao makuu na Ikulu ya Dodoma ikakamilika, ujenzi wa madarasa na ununuzi wa madawati, vifaa tiba na mashine za kupima magonjwa kupelekwa hadi ngazi ya kituo cha afya, Daraja la Busisi, madaraja mengi katika nchi hii likiwamo la Kalebe-Kihanja, Bukoba, mpango wa nishati safi (nitaeleza manufaa kadri tunavyosonga)… ni wazi yanatueleza Samia ni nani.

Sitanii, mama huyu kila alichojaribu kimekuwa. Leo anatueleza kupitia Ilani ya CCM ya 2025 – 2030 nia ya kujenga kongani za viwanda kila wilaya nchini. Hili ni jibu la ajira kwa vijana. Dira ya Taifa 2050 inaweka malengo makubwa ya nchi hii kuwa na uchumi wa kati wa juu kwa thamani ya dola trilioni moja, huku pato la kila Mtanzania likifikia dola 7,000 ifikapo mwaka 2050.

Lipo tusilolisema. Na hili yanipaswa kulisema kwa umakini mkubwa. Tundu Lissu yuko ndani kwa kesi ya uhaini, mimi sitaki kulijadili hili ila naomba kwa unyenyekevu mkubwa tukisome kifungu cha 39 cha Kanuni ya Adhabu kama ilivyorekebishwa mwaka 2002, kisha turejee matamshi ya Lissu na tutoe hukumu kila mtu kivyake bila kushawishiwa na tugeuze upande wa pili wa shilingi iwapo Lissu angekuwa madarakani akaibuka mtu akatoa kauli sawa na aliyoitoa ingekuwaje. Narudia, kesi iko mahakamani sitalijadili hili.

Ukiacha hilo, uhuru wa kujieleza umerejea. Nikisema, uhuru wa kujieleza haimaanishi uhuru wa kutoa kauli nje ya mipaka ya kisheria. Ukitaka kufahamu hilo, rejea mwenendo wa Jumuiya ya Ulaya, Marekani (inayotajwa kuwa Baba wa Demokrasia) na Ukraine kinachoendelea. Weka rula upime viwango vya demokrasia nchini Ufaransa pale mwanasiasa mwenye mlengo wa kulia, Marie Le Pen alipotangaza hadharani kuwa kuanzia sasa anaanzisha sera ya kubagua wageni nchini humo. Kwamba Ufaransa ni ya wazawa. Mwaka 2027 hatagombea urais wa Ufaransa. Fatilia ujue ni kwa nini.

Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume, wameijenga nchi kwa kwa jasho na damu. Wametuunganisha Watanzania kutoka Nkasi hadi Mkunya. Kutoka Niliendele hadi Kiraracha. Kutoka Rombo hadi Kyaka. Kutoka Mto wa Mbu hadi Tukuyu na Tunduma. Nchi zinaomba Mungu kufikia hapa tulipo, sisi tunataka kuuchana mkeka tulioukalia. Anaibuka Humphrey Polepole na falsafa za kubomoa nchi polepole, kisha baadhi yetu wanamshangilia. Chura alipata kuwambia watoto wakiwa wanarusha mawe mtoni, akasema: “Mchezo wenu ni mauti yetu.”

Sitanii, tupambane kulinda demokrasia, utawala wa sheria, tudai Katiba mpya, lakini jambo moja tufahamu si lazima haya yafanyike kwa kuvuruga amani, upendo na mshikamano wa Watanzania. Tunaweza kuyafanya yote haya na Tanzania ikabaki salama. Mwaka 2015 CHADEMA ilifikisha zaidi ya wabunge 100, hakuna aliyeita watu waingie barabarani. Iweje leo tuanze kuacha kuthamini maisha ya watu tuwatumie kama ngao kufikia malengo yetu?

Narudia na nahitimisha. Rais Samia kwa kuchukua fomu ya kugombea urais na Balozi Nchimbi kuwa Mgombea Mwenza, si tu wameandika historia, bali wawili hawa ni watu ambao kwa mtazamo wa wengi si watu wa visasi, ni watu wenye  maono, ni watu wanaoifahamu nchi, ni watu wanaosikiliza na mwisho wa siku ni wapenda maendeleo. Rais Samia kumbuka maneno ya Mwalimu Nyerere na yule kijana aliyegeuka nguzo ya chumvi kwa kuangalia nyuma baada ya kielelza “Huyo, huyo, huyoo, huyooo… “ Jipe moyo. Songa mbele. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827