Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imefuta vyama vyote vya siasa na kufuta mfumo wa kisheria uliokuwa unasimamia uendeshaji wake, kwa mujibu wa amri iliyoidhinishwa na baraza la mawaziri la taifa hilo la Afrika Magharibi siku ya Alhamisi.
Hatua hiyo, iliyochukuliwa na utawala huo wa kijeshi chini ya Rais Ibrahim Traoré aliyeingia madaraka kupitia mapinduzi ya Septemba 2022, ni hatua ya hivi karibuni ya kuimarisha udhibiti wa mamlaka baada ya kusimamishwa kwa shughuli za kisiasa kufuatia mapinduzi hayo.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burkina Faso, Emile Zerbo, alisema uamuzi huo ni sehemu ya juhudi pana za “kuijenga upya dola”, akidai kuwa mfumo wa vyama vingi ulikuwa unatumika vibaya na kushindwa kufanya kazi ipasavyo.
Alisema tathmini ya serikali imebaini kuwa kuongezeka kwa idadi ya vyama vya siasa kulichochea migawanyiko na kudhoofisha mshikamano wa kijamii.
Kabla ya mapinduzi, Burkina Faso ilikuwa na zaidi ya vyama vya siasa 100 vilivyosajiliwa, huku 15 kati ya hivyo vikiwa na uwakilishi katika bunge baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Amri hiyo inafuta vyama vyote vya siasa na miungano ya kisiasa. Sheria ya kufuta kanuni zilizokuwa zinasimamia vyama, ufadhili wake, pamoja na hadhi ya kiongozi wa upinzani, itapelekwa kwenye baraza la mpito kwa ajili ya kuidhinishwa, kulingana na kumbukumbu za kikao cha baraza la mawaziri.
Mali zote za vyama vilivyovunjwa ama kufutwa zitahamishiwa mikononi mwa serikali.
Taifa hilo la ukanda wa Sahel, kama zilivyo nchi jirani za Mali na Niger, limekuwa likipambana na mashambulizi ya makundi ya wanamgambo wa Kiislamu yanayohusishwa na al-Qaeda na Islamic State, ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwafanya mamilioni kukimbia makazi yao katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.


