Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini tangazo la kupiga marufuku raia wa mataifa 12 kuingia nchini humo. Katika awamu yake ya kwanza Trump aliwazuia watu kutoka mataifa saba yenye Waislamu wengi kuingia Marekani.

Vyombo vya habari va nchini Marekani vimeripoti taarifa hiyo vikiwanukuu maafisa wa utawala wa Trump siku ya Jumatano.

Tangazo linawazuia kabisa na kuwawekea mipaka raia wa mataifa hayo kuingia nchini Marekani. Mataifa hayo ni Afghanistan, Myanmar, Chad, Kongo, Guinea ya Ikweta, Eritrea, Haiti, Iran, Libya, Somalia, Sudan na Yemen, hii ikiwa ni kulingana na kituo cha utangazaji cha CBS.

Aidha raia wa mataifa mengine saba ya Burundi, Cuba, Laos, Sierra Leone, Togo, Turkmenistan na Venezuela watawekewa zuio la kiwango fulani, limeripoti CBS.

Wakati wa muhula wake wa kwanza, Trump aliwapiga marufuku wasafiri kutoka mataifa saba yenye idadi kubwa ya Waislamu kuingia Marekani, hatua ambayo hata hivyo ilipata ukinzani wa kisheria.

Hatua hiyo lakini ilibatilishwa na Rais Joe Biden mnamo mwaka 2021, akisema imelitia doa taifa hilo.

Katika hatua nyingine, Trump ameagiza uchunguzi kuhusu kile ambacho wanasiasa wa chama chake cha Republican wanadai kuwa ni kufichwa kwa hali ya afya ya mtangulizi wake Joe Biden alipokuwa madarakani.