Rais wa Namibia, Dk Netumbo Nandi-Ndaitwah (73) anatarajia kuwasili nchini leo kwa ziara ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Ziara hiyo ni ya kwanza ya Rais huyo tangu aapishwe kuiongoza Namibia Machi 21 mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Shaaban Kissu ziara hiyo inalenga kukuza ushirikiano wa kisiasa, uchumi na kijamii katika nyanja za biashara, uwekezaji na elimu.

“Tanzania na Namibia zimejenga uhusiano wa muda mrefu wa kindugu na kidiplomasia hivyo ziara hiyo itafungua fursa mpya za ushirikiano zitakazowezesha wananchi wa nchi zote mbili kunufaika kiuchumi,” alisema Kissu kwenye taarifa yake.

Akiwa nchini, Rais Nandi- Ndaitwah atatembelea kituo cha urithi na ukombozi wa Afrika na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama sehemu ya kuthamini mchango wa kihistoria wa Tanzania katika harakati za ukombozi Afrika na pia kukuza ushirikiano wa kielimu na kitamaduni kati ya Tanzania na Namibia.