Rais wa zamani wa Zambia Edgar Lungu (68) amefariki dunia katika hospitali moja nchini Afrika Kusini, chama chake cha Patriotic Front kimesema.
Lungu alikuwa kiongozi wa taifa hilo la Kusini mwa Afrika kati ya 2015 na 2021, aliposhindwa kwenye uchaguzi na kiongozi wa upinzani wa muda mrefu na Rais wa sasa Hakainde Hichilema.
“Rais wa zamani, ambaye amekuwa akitibiwa nchini Afrika Kusini, amefariki dunia tarehe 5 Juni, siku ya Alhamisi,” Chama cha Patriotic Front kimesema kupitia taarifa kwenye mtandao wa Facebook.
Chama hicho pia kimeweka video ya binti yake Lungu,Tasila Lungu, ambaye ni mbunge nchini Zambia, akitangaza kifo cha babake.
“Baba yangu… katika wiki za hivi karibuni amekuwa akitibiwa. Hali yake ilikuwa chini ya uangalizi mzuri na wa heshima,” alisema.
Lungu alichukua uongozi wa nchi 2015 baada ya kifo cha aliyekuwa rais wakati huo Michael Sata. Kisha akashinda uchaguzi uliomuweka madarakani kuanzia Agosti 2016 hadi Agosti 2021.
Mwanasheria huyo pia aliwahi kuwa waziri wa sheria na waziri wa ulinzi.
Baada ya kushindwa 2021, Lungu alistaafu, kisha akarejea tena kwenye siasa 2023, na kukubaliwa kama kiongozi na mgombea wa urais wa muungano wa upinzani ikiwemo chama cha Patriotic Front.
Lakini mwezi Desemba mwaka jana, mahakama ya katiba ya Zambia iliamua kuwa haruhusiwi kugombea kwa muhula mwingine tena.
