Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka Wamachinga kuondokana dhana ya kuwa Serikali inawafukuza maeneo ya biashara ila sehemu ya kuhakikisha wanafungua Barabara zinapitika na usafiri wa umma hauathiriwi ili kupunguza msongamano na foleni katikati ya Jijini.

‎Akizungumza leo Machi 2,2026 Jijini Dar es Salaam RC Chalamila amesema taarifa hiyo imekuja hivi Karibuni baada ya malalamiko kutoka kwa wananchi na madereva wa bodaboda kuhusiana na shughuli za wafanyabiashara ambazo mara nyingine hufunga barabara na kusababisha msongamano mkubwa.


‎Amesema ongezeko la kuachia barabara, hususan katika eneo la Kariakoo, limekuwa changamoto kwa Wasafirishaji wa bidhaa wanatumia Magari,Pikipiki bajaji na maguta pia kukosa usalama wa abiria hivyo wamachinga wanasisitizwa wafanye biashara zao, lakini barabara lazima wahakikishe zinapitika vizuri.

“Machinga hawatafukuzwa kwenye maeneo yao, lakini wafanyabiashara wote wanatakiwa kufanya biashara bila kufunga barabara kwani hii sehemu ya juhudi za kuhakikisha usafirishaji na usafiri wa umma hauathirikiwi”amesisitiza Chalamila

‎Kampeni maalum za kufungua barabara zimeshaanza katika baadhi ya mtaa na vijiji vya jiji, ambapo watendaji wa serikali wanashirikiana na wafanyabiashara kuhakikisha njia za usafiri zinabaki wazi. Lengo ni kuunganisha maendeleo ya biashara na utaratibu wa usafirishaji.

‎Wafanyabiashara wanahimizwa kushirikiana na serikali na kufungua barabara bila kuchelewesha shughuli zao. Chalamila aliwataka wananchi na wafanyabiashara kuelewa kuwa hatua hii ni kwa manufaa ya wote, ili kupunguza msongamano na kushirikiana katika usalama wa barabara.

‎Aidha, serikali ya mkoa inatazamia kuendeleza kampeni hizi katika maeneo mengine ya jiji, kuhakikisha usafiri wa umma unakuwa wa uhakika na wafanyabiashara wanaweza kufanya biashara zao kwa huru bila kuzuiwa.

Hata hivyo amebainisha kuwa kumekuwa na Changamoto ya foleni hivyo wananajitahidi Kupitia maandiko Mbalimbali ili kusaidia kuleta Suluhu ya kudumu hivyo Wananchi wawe wapole

Aidha RC Mhe Albert Chalamila ametoa muda wa wiki moja kuanzia machi 2,2026 kwa makundi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya utapeli na unyang’anyi wa mali ikiwemo ardhi kujisalimisha kwa kurudisha mali walizozichukua kwa wamiliki halali kwani Serikali mkoani humo imekusidia kuchukua hatua kali za kisheria kwa wote watakaokiuka agizo hilo

“Hivi Karibuni nilifanya Ziara Mkoa wa Dar es salaam wilaya ya Kinondoni kubaini kukithiri kwa vitendo hivyo ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakitumia njia ya kukodisha maeneo na baadae kufanya utapeli nilibaini uwepo wa kiwango kikibwa cha utapeli na unyang’anyi wa ardhi na kusababisha vilio na machozi kwa baadhi ya makundi ya watu ikiwemo wajane na warithi” amesema RC

RC Chalamila ameongeza kuwa Serikali Mkoani humo pia imebaini uwepo wa utapeli kwenye show room za kuuzia magari ambapo watu wamekuwa wakilipia magari na kudhulumiwa kwa kisingizio kuwa magari yao bado yapo bandarini lakini pia Serikali imebaini uwepo wa mikopo isiyokuwa na tija inayowaumiza wananchi kupitia masharti magumu hivyo anakwenda kuchukua hatua

Sanjari na hayo RC Chalamila ameipongeza Mahakama na TAKUKURU kwa namna wanavyoshugulikia kesi hizo huku akitoa tahadhari kwa baadhi ya wasimamizi wa mirathi wanaouza mali za warithi halali kwa kisingizio cha kulea ama kisomesha watoto wa marehemu kwani yapo matukio mengi ya warithi kunyimwa haki zao.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa Mhe Albert Chalamila amezungumzia ujio wa Rais Dokta Samia Suluhu Hassan katika Mkoa huo machi 3, 2026 ambapo anatarajia kuzindua matanki ya kuhifanyia mafuta wilaya ya kigamboni hivyo amewataka wananchi kukitokeza kwa wingi kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania