Na Mwandishi Wetu, JamhuriMesia, Singida

Katika nchi inayokumbwa na changamoto za kiafya, mazingira na umasikini, nishati safi ya kupikia si tu hitaji la msingi bali ni kichocheo cha maendeleo ya kweli kwa watu na Taifa kwa ujumla.

Katika kukabiliana na ukataji miti ambapo takribani asilimia 16 ya eneo la nchi tayari limegeuka kuwa janga, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ilizindua mkakati wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya watu wanaachana na matumizi ya kuni na mkaa ifikapo mwaka 2034.

Akizungumza ofisini kwake leo tarehe 23 Februari 2026 mara baada ya kupokea ujumbe wa wataalamu kutoka Wakala wa Nishati Vijijini – REA waliopo mkoani Singida kwa ajili ya kuutambulisha mradi wa uuzwaji wa majiko banifu kwa bei ya ruzuku, Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara katika utekelezaji wa mkakati wa nishati safi ya kupikia.

Vilevile Mhe Dendego amesema kuwa Rais Samia ni kinara wa utekelezaji wa Nishati safi Afrika hivyo mkoa wa Singida upo tayari na utaanza kugawa majiko hayo banifu katika wilaya zote za mkoa wa Singida ili mpaka kufikia mwaka 2030 mkoa huo uwe umetengeneza alama kubwa kwa wananchi wake kabla hata ya kufikia mwaka 2034.

Pia, amesema kuwa mkoa wa Singida umepokea mitungi ya gesi zaidi ya 18,000 ambayo imesambazwa kwa wananchi ili kutokomeza kabisa nishati chafu ya kupikia.

Kwa upande wake Mhandisi Raya Majallah kutoka REA-Idara ya Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida ameutambulisha mradi wa uuzwaji wa majiko banifu kwa bei ya ruzuku katika mkoa huo ambapo amesema kuwa Wakala wa Nishati Vijijini umeandaa mpango huo wa uuzaji wa majiko banifu 200,000 kwa bei ya ruzuku yenye ufanisi mkubwa katika utumiaji wake.

Mradi huo unahusisha usambazaji wa majiko banifu yanayotumia kuni na mkaa kidogo ili kupunguza matumizi ya vyanzo hivyo vya nishati Pamoja na athari za moshi zitokanazo na matumizi katika majiko ya kawaida.

Mhandisi Majallah amesema kuwa mikataba hiyo ilisainiwa Mei 9, 2025 na itatekelezwa ndani ya miezi 15 ambapo gharama ya mradi huo ni Shilingi Milioni 340,288,200 kwa mkoa wa Singida na ruzuku inayotolewa na wakala wa nishati vijijini-REA ni shilingi milioni 289,230,504.47 sawa na asilimia 85 ya gharama ya mradi huku wananchi wakichangia Shilingi 51,057,691.53 sawa na asilimia 15 ya gharama ya mradi.