Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, amehudhuria sherehe ya Mahafali ya 60 ya Chuo cha Elimu ya Biashara ‘College of Business Education (CBE)’ Kampasi ya Dodoma na kuwatunuku Wahitimu 2,086 wa mwaka 2025 shughuli iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kituo cha Jakaya Kikwete.
Mhe. Senyamule amesema Serikali ya awamu ya sita katika kipindi hiki kifupi imeboresha na kuimarisha Elimu ya vyuo vikuu na vile vya kati ili kuwawezesha Wahitimu kupata soko huru la ajira sambamba na kuongeza Wataalam ndani ya nchi watakaoweza kutoa majawabu ya changamoto mbalimbali.
“Sisi tunaamini yote haya yamefanyika ili kuongeza idadi ya Watanzania ambao wana uwezo wa kutoa majawabu ya changamoto zao wenyewe, jamii na za nchi yetu kwa ujumla lakini pia haya yataleta ushindani kwa soko la ajira hasa ninyi muliohitimu elimu ya chuo, mnaweza kwenda kuajiriwa nchi yeyote kulingana na uwezo na cheti chako”.
Mhe. Senyamule ameongeza kuwa Serikali imetengeneza mazingira rafiki ya kujiajiri kutokana na ufinyu wa nafasi za ajira kwa kuboresha miundombinu mbalimbali kama barabara, SGR, kusambaza umeme katika kila kijiji ambapo vyote hivyo vinaweza kutumika kama fursa za ajira kupitia shughuli nyingi za kiuchumi zinazoweza kuanzishwa kwayo.
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa chuo hicho Profesa Zakaria Mganilwa ametaja jukumu kubwa linalosimamiwa na Bodi yake kuwa ni kuhakikisha Mifumo bora ya uwajibikaji kwa Wakufunzi na wanafunzi inafuatwa ili kutimiza lengo la kuanzishwa kwa Taasisi hiyo ambalo ni kupata wataalam mahiri wa fani za Biashara watakaotumika ndani na nje ya nchi.
Vilevile, Mkuu wa Chuo hicho Profesa Edda T. Lwoga, amesema tangu kuanzishwa Chuo hicho Januari 21, 1965 na Mwalimu Julius Nyerere, kimeendelea kuwa bora kwenye utoaji wa kozi za Biashara na kimekua kikianzisha mitaala mipya kila wakkulingana na mahitaji ya soko ambayo inawezesha kutoa Wataalam Wabobevu kwenye sekta hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Wahitimu, Bi. Irene Mtui amesema ujuzi alioupata katika chuo hicho utamsaidia katika shughuli zake na ametoa wito kwa Wahitimu wenzake kuzingatia Hotuba ya Mgeni rasmi inayowataka kutumia fursa zilizopo kujiajiri hususan katika Mkoa wa Dodoma ambao ni Makao Makuu ya nchi ili ujuzi wao usipotee bure.




