📍NIRC Iringa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amewataka Wahandisi wa Mikoa na Wasimamizi wa miradi ya Umwagiliaji nchini kufanya kazi kwa uzalendo wa hali ya juu na weledi ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali unaleta tija iliyokusudiwa kwa wananchi.
Mhe. James ameyasema hayo mkoani Iringa wakati akifunga mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo watumishi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) yaliyohusu Usimamizi wa Mikataba, Sheria za Ununuzi, Uhandisi wa Geoteknolojia (Utafiti wa Miamba) na ubadilishanaji wa uzoefu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. James amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa miongozo na fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha sekta ya Umwagiliaji , akibainisha kuwa miradi hiyo ni tegemeo kubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kukuza uchumi wa taifa.
“Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza fedha nyingi; ni matarajio yetu kuwa miradi hii itatekelezwa kwa wakati, kwa viwango na ubora unaotakiwa. Mafunzo haya yamekuja wakati mwafaka ili kuwawezesha kusimamia rasilimali hizi zinazotokana na kodi za wananchi,” alisema Mhe. James.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ameipongeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji chini ya Mkurugenzi Mkuu, Raymond Mndolwa, kwa kuimarisha weledi na kudhibiti migogoro inayokwamisha miradi.
Amesisitiza kuwa bila msimamo wa kusimamia weledi, miradi mikubwa ikiwemo ile ya mabilioni ya fedha kama mradi wa Mkombozi ingebaki kuwa hadithi badala ya kuleta matokeo.

“Sisi ndio ‘trigger’ ya mabadiliko kupitia kilimo. Kupitia kazi yenu, mnakwenda kutengeneza ajira za vijana na kuitambulisha Tanzania kwenye biashara ya chakula duniani. Msifanye viongozi wawe na kigumizi mbele ya wananchi; wapeni ujasiri kwa kutimiza majukumu yenu kwa wakati,” alisisitiza.
Pia amewataka wahandisi hao kutanguliza uzalendo katika utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji, akisisitiza kuwa miradi hiyo ni mali ya Watanzania wote na inapaswa kukamilishwa kwa uaminifu na kujituma.
RC James amesema uzalendo wa wahandisi unaonekana katika kusimamia miradi kwa umakini, kuzingatia muda wa utekelezaji na kuhakikisha thamani ya fedha za umma inalindwa katika kila hatua ya mradi.
“Na Serikali ina maono makubwa ya kuimarisha kilimo cha umwagiliaji, hivyo mafanikio ya maono hayo yanategemea sana dhamira ya wahandisi katika kukamilisha miradi kwa viwango vinavyotakiwa,” amesema RC James.

Mkuu huyo wa mkoa wa Iringa amewakumbusha washiriki kuwa mipango yote ya maendeleo ina muda maalum wa utekelezaji, na uzalendo wa kweli unaonekana pale watumishi wanapohakikisha miradi inakamilika kwa wakati bila visingizio.
Mkuu huyo wa mkoa wa Iringa amewakumbusha washiriki kuwa mipango yote ya maendeleo ina muda maalum wa utekelezaji, na uzalendo wa kweli unaonekana pale watumishi wanapohakikisha miradi inakamilika kwa wakati bila visingizio.
Hata hivyo, Mhe. James ameahidi kuwa uongozi wa Mkoa wa Iringa utaendelea kushirikiana kwa karibu na Tume hiyo kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa mkoani humo inakamilika na kuwanufaisha wananchi kama ilivyopangwa.
Mafunzo hayo yaliwashirikisha Wahandisi wa Umwagiliaji wa mikoa, Menejiment, Wataalamu wa kada mbalimbali na Wasimamizi wa miradi kutoka maeneo mbalimbali nchini, yakiwa na lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa amesema Tume imejipanga kusimamia miradi ya umwagiliaji kwa karibu ili kuhakikisha inakamilika kwa ufanisi na kuleta tija kwa wakulima na taifa kwa ujumla.
Mndolwa amesema NIRC inaendelea kujenga mabwawa ya Umwagiliaji, kuvuna na kuhifadhi maji pamoja na kutekeleza shughuli za uhifadhi wa mazingira, akieleza kuwa hatua hizo ni sehemu ya uzalendo wa kulinda rasilimali za Taifa ili kufikia adhima ya kuongeza uzalishaji wa mazao na kujitosheleza kwa chakula cha ndani na kuilisha Dunia.
“Na katika kulinda mazingira ya miradi, Tume imefanikiwa kupanda miti mingi katika maeneo mbalimbali na ujengaji wa mabwawa, hatua inayolenga kuhifadhi vyanzo vya maji na kuhakikisha miradi inadumu kwa muda mrefu,” amesema Mndolwa
Washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Rie wa Mkoa wa Morogoro Juma Matanga amesema washiriki hao wamepata uelewa mpana kuhusu wajibu wao kama kwa mikoa yote nchini, wakiahidi kutumia maarifa waliyopata kukamilisha miradi ya Umwagiliaji ipasavyo kwa kuzingatia weledi, uwajibikaji na uzalendo.






