Na WMJJWM- Kilimanjaro

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu amewataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mkoani humo kuwajibika kwa jamii kwa kuhakikisha mipango yao inasaidia kutatua changamoto zilizopo katika jamii.

Mhe. Babu ameyasema hayo Juni 24, 2025 wakati akifungua Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa mkoa wa Kilimanjaro linaloongozwa na Kaulimbiu isemayo: Tathmini ya Mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya Taifa 2020/2021-2024/2025; Mafaniko, Changamoto, Fursa na Matarajio.

Amesema Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni mkono wa pili wa Serikali kwani yanasaidia katika kutoka huduma mbalimbali kwa jamii kupitia miradi wanayotekeleza.

“Niwaombe mfanye kazi kwa kutekeleza majukumu yenu katika kuisaidia jamii inayowazunguka, mnapokea pesa kutoka kwa wafadhili mbalimbali kwasababu ya Watanzania hivyo inabidi mkatatue changamoto zao” amesema Mhe. Babu

Ameongeza kuwa Serikali imeweka mazingira mazuri ya utendaji kazi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika mikoa na Halmashauri ili kuhakikisha NGOs zinafanya kazi zao za kuihudumia jamii kwa kuunga mkono juhudi za Serikali kuleta maendeleo kwa jamii.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Kiseo Yusuf Nzowa amesema Mkoa utaendelea kushirikiana na Mashirika hayo katika kuleta maendeleo kwa jamii kupitia Miradi mbalimbali na kufuatilia kwa ukaribu utendaji kazi wa Mashirika hayo mkoani humo.

Akitoa salamu za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Msajili wa NGOs Francisca Mwendesha amesema Mashirika hayo yanatakiwa kufanya kazi zake kwa kuzingatia Sheria, taratibu na miongozo iliyopo katika utekelezaji wa mipango na mikakati yao katika kuihudumia jamii.

Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACoNGO) Mkoa wa Kilimanjaro Adam Mwamshambo amesema Baraza litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha NGOs zinatekeleza mipango na mikakati yake kupitia Miradi mbalimbali katika kuisaidia jamii kwa kutatua changamoto zao katika nyanja mbalimbali.