Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia, Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amewaasa baadhi ya viongozi na watendaji kuondoa ukiritimba unaowakimbiza wawekezaji na wananchi wanaohitaji huduma, akisema vitendo hivyo vinakatisha tamaa na kurudisha nyuma maendeleo.

Aidha, amesema ni muhimu viongozi na watendaji wa serikali kuanzia ngazi ya chini, wilaya hadi mkoa kuwajibika ipasavyo katika maeneo yao ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Kunenge alitoa kauli hiyo Disemba 11, 2025 wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha watendaji na viongozi mbalimbali wa mkoa huo kwa lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa ahadi za siku 100 za kwanza za uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alifafanua kuwa, ingawa Rais Samia aliahidi mambo kadhaa, yapo masuala ya kisera pamoja na mengine yanayopaswa kutekelezwa katika ngazi ya mkoa, wilaya, halmashauri na manispaa.

“Tumekubaliana kuhusu vipaombele,mikakati ya utekelezaji, hatua hii itatusaidia ifikapo siku hizo kuhakikisha mambo muhimu tumeyafikia “:;Vipaumbele viwekwe sahihi kwa maendeleo yenye matokeo chanya,” alisisitiza Kunenge.

Vilevile, alisema katika kujenga uchumi wa kujitegemea kupitia fedha za ndani, kila wilaya inapaswa kuongeza mapato ya ndani sambamba na kuimarisha uwekezaji, hatua ambayo itafanikiwa endapo urasimu utapunguzwa.

Katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, walimkabidhi tuzo Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoani Pwani, Injinia Baraka Mwambage, kwa kutambua utendaji wake bora.

Kunenge alibainisha ,Injinia Mwambage ametekeleza majukumu makubwa mwaka huu na kuwa mfano wa kuigwa, hivyo mkoa umetambua mchango wake mkubwa katika kuinua sekta ya miundombinu.

Kwa upande wake, Injinia Baraka alishukuru kwa heshima hiyo, akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na kufanya kazi kwa ushirikiano na kwenda sambamba na kasi ya maendeleo inayosimamiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.