Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa katika kuchochea sekta ya uwekezaji na biashara, huku akitoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje kufika kuwekeza katika Manispaa ya Mji wa Kibaha.

Ameeleza kuwa Kibaha Mjini sasa imepanda hadhi na kuwa Manispaa, ikiwa na maeneo mengi yanayofaa kwa uwekezaji katika biashara, viwanda na kilimo.

Kutokana na hilo, Serikali itaongeza juhudi za kuhamasisha ujenzi wa mahoteli ya kisasa yenye viwango vya kimataifa.

Akizungumza Septemba 4, 2025, wakati wa uzinduzi wa The Meiborn Hotel inayomilikiwa na mwekezaji mzawa, Fikirini Mushi, Kunenge alisema Kibaha Mjini imepiga hatua kubwa kimaendeleo na kiuchumi, na sasa ni miongoni mwa maeneo yanayovutia kwa uwekezaji.

“Kwa upande wa Serikali, tunaweka mkazo mkubwa katika ujenzi wa mahoteli makubwa, Tumeona maendeleo kwenye sekta ya viwanda na kilimo, lakini bado kuna changamoto ya upungufu wa mahoteli yenye hadhi ya kimataifa,” alieleza Kunenge.

Aidha, alimpongeza mwekezaji huyo kwa kuanzisha hoteli hiyo kwa wakati muafaka, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kumuunga mkono na kuhakikisha miundombinu ya kufika eneo hilo inaboreshwa ili kuvutia wageni.

“Tunashukuru kwa uwekezaji huu, Serikali itahakikisha eneo hili linapata miundombinu bora ili watu waweze kufika kwa urahisi, kulala, na kupata huduma bora za chakula na malazi,” aliongeza Kunenge.

Kwa upande wake, Mushi alisema ujenzi wa hoteli hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza sekta ya biashara na huduma.

Alieleza kuwa kwa sasa hoteli hiyo ina vyumba 34, kila kimoja kikiwa na gharama ya Shilingi 120,000 kwa siku, na wamejipanga kutoa ajira kwa wazawa katika maeneo mbalimbali ya hoteli hiyo.