Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMesia, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ametoa Rai kwa viongozi na watendaji wa Serikali mkoani humo kufanya kazi kwa mshikamano, mtazamo mmoja na kuzingatia vipaumbele vya Mkoa ili kufanikisha utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa ufanisi.
Aidha amesisitiza watendaji wa Serikali kupunguza urasimu katika utekelezaji wa majukumu yao, kufanya kazi kwa ushirikiano .
Kunenge aliyasema hayo wakati akifungua kikao kazi maalum kilichowakutanisha viongozi na watendaji wa Serikali kutoka Sekta mbalimbali kilicholenga kutoa muongozo na maelekezo ya utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

Alisema kikao hicho kimefanyika wakati Serikali ikiwa ndani ya siku 100 tangu Mheshimiwa Rais ateuliwe, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu na kuhakikisha malengo yaliyopangwa yanafikiwa kwa wakati.
“Tupo ndani ya siku mia moja tangu Mheshimiwa Rais ateuliwe, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunatekeleza majukumu ya Serikali kwa pamoja, kwa mshikamano na kwa maslahi mapana ya wananchi,” alifafanua Kunenge.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa alizitaka baadhi ya Halmashauri kuongeza wigo wa mapato ya ndani kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato, akieleza kuwa utegemezi wa vyanzo vya zamani ambavyo havina tija ya kutosha unakwamisha maendeleo ya Halmashauri.
Kuhusu suala la utawala bora, Kunenge alisisitiza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria, akiwataka viongozi na watendaji kuheshimu mihimili yote mitatu ya dola ili kudumisha haki, uwajibikaji na utawala wa sheria.

Kikao hicho kimefanyika January 8,2026 katika Ukumbi wa Destiny uliopo Manispaa ya Kibaha na kimehudhuriwa na viongozi wa Mkoa na Wilaya, watendaji wakuu wa Serikali, wawakilishi wa taasisi wezeshi pamoja na Waheshimiwa Madiwani.




