. _Lengo ni kujitambulisha na kuomba ushirikiano
. Asema ushirikiano wa serikali na Taasisi za dini ni muhimu.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA Amos Makalla Leo Jumatatu Septemba Mosi, 2025 amefanya ziara ya kuwatembelea viongozi wa Dini Mkoani Arusha kwa lengo la kujitambulisha na kubadilishana uzoefu katika mambo mbalimbali.
Ziara ya mkuu wa mkoa ni muendelezo wa ziara zake za kujitambulisha na kupata taarifa za taasisi mbalimbali katika mkoa wa Arusha.

Katika ziara hiyo kwa Askofu wa tatu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati Askofu Dkt. Godson Abel Mollel, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Sheikh Shaaban Juma Abdallah na Nabii Mkuu Dkt. GeorDavie M. K wa Kanisa la Ngurumo ya Upako, Mhe. Makalla amewaomba pia Viongozi hao ushirikiano pamoja na kuliombea Taifa la Tanzania ili liendelee kuwa na Amani na utulivu.
Kwa upande wao Viongozi hao wa dini, mbali ya kumshukuru Mhe. Makalla kwa kuwatembelea, kujitambulisha na kuomba ushirikiano nao, wameahidi kumpatia ushirikiano wa kutosha katika kuwatumikia wananchi wa Mkoa wa Arusha, wakiahidi kuendelea kuhubiri kuhusu amani, upendo na mshikamano wa jamii hasa wakati huu ambapo Taifa linaendelea na Kampeni kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Viongozi hao wa dini kadhalika walipata fursa ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM pamoja na wasaidizi wake wote ili Mungu aendelee kuwapa baraka, hekima, maarifa na utashi zaidi katika kuwaletea watanzania maendeleo.



