Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewataka wakandarasi wanaotekeleza mradi wa usambazaji wa mifumo midogo ya umeme jua katika maeneo ya visiwani kuhakikisha wanatumia muda vizuri na kukamilisha kazi kwa wakati, ili kuwaondolea wananchi wa maeneo hayo adha ya ukosefu wa nishati ya uhakika.

Akizungumza leo Juni 13, 2025 ofisini kwake jijini Mwanza, Mhe. Mtanda amewataka pia wataalamu kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha kuwa wakandarasi wanalipwa kwa wakati, jambo litakalowasaidia kuendelea na kazi bila kuchelewa.

“Ni muhimu kutumia muda vizuri na kukamilisha miradi hii kwa wakati. Serikali inatambua juhudi za kila mkandarasi anayefanya kazi kwa bidii na kwa ufanisi, na hao ndio wanaopewa kazi nyingine zaidi. Chema chajiuza, kibaya chajitembeza,” amesema RC Mtanda.

Mkuu huyo wa mkoa pia amewasisitizia wakandarasi umuhimu wa kujitambulisha kwa mamlaka za mikoa, wilaya, tarafa na vijiji ili jamii ziwe na uelewa wa mradi huo, kushirikishwa kikamilifu na kutoa maoni, taarifa au mapendekezo yatakayosaidia kufanikisha utekelezaji wake.

“Kwa kufanya hivyo, mtapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi. Na pale changamoto zinapojitokeza, ni rahisi kupata msaada au taarifa muhimu kutoka kwao,” aliongeza.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Ernest Makale, amesema mradi huo wa umeme wa jua unatekelezwa katika visiwa 78 vilivyopo wilaya tano za Mkoa wa Mwanza ambazo ni Sengerema, Buchosa, Ukerewe, Magu na Ilemela.

Mhandisi Makale Pia amebainisha kuwa zaidi ya shilingi bilioni 4 tayari zimetengwa kwa ajili ya mradi huo, ambao unalenga kufikisha huduma ya umeme katika nyumba takribani 8,410 kwa bei ya ruzuku ya mpaka asilimia 75.

Lengo kuu la mradi huo ni kuhakikisha kuwa wakazi wa maeneo ya visiwani wanapata huduma ya nishati ya umeme ya uhakika, jambo litakaloboresha maisha yao na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo husika.