Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Songea
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas,amefungua Maktaba ya Mkoa wa Ruvuma baada ya kusimama kutoa huduma kwa miaka mitatu mfululizo kutokana na uchakavu wa majengo yake.
Akizungumza na wanafunzi,wananchi na wafanyakazi wa idara na taasisi za Serikali na watumishi wa Bodi ya Huduma za maktaba Brigedia Jenerali Abbas,amewataka wanafunzi,walimu na wadau wa elimu kutumia maktaba hiyo kama Daraja la kufikia mafanikio na vijana kukuza ubunifu,utafiti na mawazo mapya.
Abbas aliwataka wazazi na walezi Mkoani Ruvuma,kuwahimiza watoto wao kupenda kusoma vitabu na kutumia muda wao katika shughuli za maarifa.

Alisema,kufunguliwa upya kwa maktaba ya Mkoa wa Ruvuma ni ishara ya dhamira ya kweli ya Serikali ya awamu ya sita kupitia Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania(TLSB) kuendeleza elimu,kujenga jamii inayotumia maarifa na kuandaa Tiafa lenye uwezo wa kushindana katika karne ya 21.
Alisema, kwa kufanya ukarabati huo Serikali imeonesha kwa vitendo kwamba maktab ani nyenzo muhimu ya kupunguza pengo la maarifa,kuongeza usawa na furs ana kujenga uchumi wa kisasa wa viwanda,ubunifu na TEHAMA.
Brigedia Jenerali Abbas alisema, tunapokusdia kutekeleza dira ya maendeleo ya Taifa 2050 tunapaswa kutambua kuwa,uchumi unaotegemea maarifa hauwezi kujengwa bila mfumo imara ya upatikanaji wa taarifa sahihi.
Kwa mujibu wa Abbas,maktaba hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuharakisha kila Mtanzania anakuwa na uwezo wa kusoma,kufanya utafiti,kujifunza teknolojia na kutumia taarifa sahihi kwa maendeleo binafsi na Taifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania Dkt Mboni Ruzegea alisema,ukarabati wa maktaba ya Mkoa wa Ruvuma ulianza mwaka 2021 kwa ushirikiano na Manispaa ya Songea kwa kusaidia kuandaa BOQ ya mahitaji halisi ambapo gharama ilifikia jumla ya Sh.247,000,000.

Dkt. Ruzegea alisema,lakini fedha zilizoletwa ni Sh.97,000,000 hali iliyofanya kazi ifanyike kwa awamu kulingana na rasilimali na kibali cha matumizi ya fedha hizo kilitoka Mwezi Agosti 2022 na ukarabati ndipo ulipoanza kwa kufanya matengenezo yap aa,kuondoa viti vya mbao,kupaka rangi ndani na nje na kufanya marekebisho ya miundombinu ya umeme.
Dkt. Ruzegea alisema,mwaka 2023 Bodi iliendelea kukamilisha vipengele muhimu kwa kutumia mapato ya ndani ikiwemo kuweka gril,vioo vya aluminiam,bustani na ujenzi wa vyoo vya nje na vyoo vya walemavu ili kurejesha mazingira salama na rafiki kwa watumiaji.
Alisema, mwaka 2023 Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania ilitenga kiasi cha Sh.37,000,000 kutoka mapato yake ya ndani ili kukamilisha kazi za mwisho kama uzio na geti,kukata vyumba kwa ajili ya ofisi(Partitions) za sehemu ya watoto na chumba cha kompyuta na ukarabati wa ofisi ya mkutubi.
“Hadi kufikia Juni 2025 ukarabati ulifikia asilimia 90 kabla ya kukamilika mwezo Oktoba na kuanza maandalizi ya ufunguzi ili huduma zirejee rasmi kwa wananchi wa Songea na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla”alisema Dkt Ruzegea.
Alisema, kwa sasa Maktaba ya Mkoa wa Ruvuma iko chini ya Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania katika uendeshaji na usimamizi wake na huduma zinazotolewa ni elimu kupitia shughuli za usomaji na utafiti,upatikanaji maarifa kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma hususani wanaoishi katika Wilaya ya Songea.
Alisema, lengo la kuanzishwa kwa Maktaba katika Mkoa wa Ruvuma ni kuhudumia wanafunzi na walimu,watumishi wa umma,watafiti na wananchi licha ya miaka ya mwanzo kuwa na upungufu wa vitendea kazi yaani vitabu na muamko mdogo wa jamii kwani awali watumiaji wengi walikuwa wanafunzi wa shule za Manispaa ya Songea na Chuo cha Ualimu Matogoro na baadhi ya wananchi wachache wenye hamasa ya kujisomea.
Dkt Ruzegea alisema,ukarabati uliofanyika unaonyesha dhamira ya kweli ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imetafsiriwa kwa vitendo kwenye uwekezaji katika elimu kupitia Maktaba za umma.
Alisema, Serikali imehakikisha inapeleka kwa Watanzania huduma za usomaji ili kukuza maarifa,ujuzi ubunifu, kupitia teknolojia,mambo ambayo ni muhimu na nguzo kubwa ya maendeleo ya Taifa lolote katika karne ya 21,mapinduzi ya 4 ya viwanda yenye sifa ujumuishi wa teknolojia za kidijitali kama Al,lot na robotiki katika tasinia mbalimbali ikiwemo elimu,afya,kilimo na mazingira.
Mkurugenzi wa uendeshaji wa huduma za maktaba Tanzania Dkt Rehema Ndumbaro alisema,kufunguliwa kwa maktaba Mkoani Ruvuma ni mwanzo mpya unaoleta matumaini,maarifa na fursa pana kwa wananchi wa Mkoa huo.
