Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas ametoa wito kwa Jeshi la Polisi Mkoani humo kuhakikisha kuwa wanatumia vitendea kazi walivyopewa yakiwemo magari kuyatumia kwa usahihi na umakini mkubwa.

Wito huo ameutoa leo kwenye hafla fupi ya kukabidhi magari 24 iliyofanyika kwenye viunga vya ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma yaliyotolewa na Serikali kwa Jeshi la Polisi mkoani humo.

Alisema kuwa magari hayo yatapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya usafiri kwa askari wanapokuwa kwenye majukumu yao ya kila siku.

” Magari haya ili yaendelee kufanya kazi ni lazima muhakikishe mnayafanyia matengenezo kila muda wa matengenezo unapofika ili viendelee kutumika sasa na hapo baadae, nafarijika kuwa kiongozi wa mkoa ambao vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi zake kwa weledi na vinatii Sheria za Nchi, pia vinakuwa tayari kushirikiana na wananchi walio wema katika kulilinda Taifa hili” alisema Mkuu huyo wa Mkoa Brigedia Jenerali Ahmed.

Alisisitiza kuwa weledi ,utii ndio kiapo cha askari wanachopaswa kuishi nacho katika majukumu yao ya kila siku na si vinginevyo.

Aidha amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuwajari askari mara kwa mara na kuwapatia vitendea kazi ambavyo vinasaidia kuwarahisishia utendaji wa kazi ndani ya Jeshi hilo.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma Marco Chilya ameishukuru serikali kwa kupitia Wizara ya mambo ya ndani pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kwa kuona umuhimu wa kutoa magari hayo ambayo katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu pamoja na shughuli zingine yatasaidia kwa kiasi kikubwa kulinda usalama wa raia wema na Mali zao.

Chilya pia ametoa wito kwa wananchi kujenga mahusiano mazuri na vyombo vya Dora ili kuendelea kudumisha amani na kusaidia kufichuwa waharifu ambao wanaweza wakahatarisha uvunjifu wa amani na kwamba magari hayo yatasambazwa kwenye Wilaya zote tano za Mkoa wa Ruvuma.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas akikagua gwaride la kikosi Cha kutuliza ghasia (FFU) kabla ya kukabidhi magari mapya 24 ya jeshi hilo.