πŸ“Œ Wananchi wasisitizwa kulinda miundombinu ya umeme

πŸ“Œ Vitongoji 1481 kati ya 2406 tayari vimefikishiwa umeme

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Lindi

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wamekabidhi rasmi Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack Vijiji vyote 523 ambavyo tayari vimefikishiwa umeme.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika leo Mei 7, 2025 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu amesema kuwa REA sasa inaendelea na kupeleka umeme katika Vitongoji.

β€œLeo ni siku ya furaha sana kwetu na kwa Wananchi wa Mkoa wa Lindi. Mkoa wa Lindi una jumla ya Vijiji 523 na vijiji vyote sasa tumeshavifikishia huduma ya umeme. Hatuna deni na Wananchi wa vijiji vya Mkoa huu,” amesema Mwenyekiti Kingu.

Ameongeza kuwa, Mkoa huo una jumla ya vitongoji 2406 na vitongoji 1481 tayari vimeshafikishiwa umeme huku vitongoji 442 wakandarasi wako wanaendelea na kazi.

Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya Mwenyekiti wa REB, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack amempongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa fedha zilizofanikisha mradi huo kukamilika kabla ya muda uliopangwa.

β€œMhe. Rais anaendelea kuonyesha nia yake ya kutamani kuwaletea maendeleo Watanzania. Tunapenda kumpongeza sana Mhe. Rais, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Watendaji wote wa Serikali waliowezesha ndoto hii kutimia,” amesema Mhe. Telack.

Ameongeza kuwa, uwepo wa umeme vijijini licha ya kuboresha huduma za kijamii katika vijiji, utasaidia kuinua uchumi wa wananchi kwa kufanya shughuli mbalimbali zitakazowaongezea kipato.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu amewaomba viongozi kuendelea kuwahamasisha wananchi kulinda miundombinu ya umeme kwa kuwa serikali imetoa fedha nyingi kufikisha umeme kwa wananchi.

β€œSerikali imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 186.4 kwa ajili ya kufikisha umeme katika vijiji vyote 523 vya Mkoa wa Lindi. Tuwaombe viongozi muendelee kuwahamasisha wananchi kulinda miundombinu hii ya umeme,” amesema Mhandisi Olotu.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Lindi, Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Lindi, Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.