
📌Rais Samia apewa kongole uhamasishaji nishati safi
📌REA, STAMICO kushirikiana uzalishaji wa Rafiki briquettes
📌Kiwanda cha Rafiki briquettes mbioni kujengwa Geita
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Geita
Wakala wa Nishati Vijijini (REA), umepongezwa na Jeshi la Magereza kwa kuhamasisha, kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 hapa nchini.
Hayo yemebainishwa na Mkuu wa Jeshi la Magereza mkoa wa Geita, ACP Jonam Mwakasagule wakati akizungumza na Bodi ya Nishati Vijijini (REB) mkoani Geita.
‘Sisi kama Jeshi la Magereza tulikuwa tunapata shida sana hasa wakati tunatumia kuni kupika na kutupotezea muda mwingi porini na kuepuka hatari za kupoteza maisha,” Amesema ACP Mwakasagule.

ACP Mwakasagule ameongeza kuwa, matumizi ya nishati safi katika jeshi hilo sasa yamepewa kipaumbe ili kujenga afya bora kwa kupunguza magonjwa ya macho na kifua yanayotokana na matumizi ya kuni wakati wa kupika chakula.
Naye, Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini Mha. Ahmed Chinemba amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 – 2034).

“Mhe. Rais amesema taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 ziachane na matumizi ya kuni na mkaa na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi asilia, umeme, bayogesi na makaa ya mawe yaliyoboreshwa, “. Amesema Mha. Chinemba.
Aidha, Mha. Chinemba ameeleza kuwa REA kwa kushirikiana na STAMICO wapo mbioni kujenga kiwanda cha kuzalisha mkaa mbadala mkoani Geita ili kurahisisha upatikanaji wa mkaa mbadala katika maeneo hayo ikiwa ni sehemu ya uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watanzania.



