📌Mradi kuzalisha kilowati 317
📌Wahariri waridhishwa na mradi wa Lupali
📌Mradi kupunguza matumizi ya nishati isiyo rafiki na mazingira
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Njombe
Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imetoa kiasi cha shilingi bilioni 5.4 kwenye mradi wa kuzalisha umeme wa maji Lupali wenye uwezo wa kuzalisha kilowati 317 unaotekelezwa na shirika la Benedictine Sisters of St. Gertrud Convent Imiliwaha.
Hayo yamebainishwa leo Machi 11, 2026 wakati wa ziara ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) walipotembelea mradi wa Lupali unaotumia nguvu ya maporomoko madogo ya maji ya mto Lupali katika kuzalisha umeme mkoani Njombe.
Akiwaeleza TEF utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Mradi kutoka REA, Mha. Emmanuel Yessaya amesema Serikali kupitia REA imetoa ruzuku kwa awamu tano zenye jumla ya shilingi za kitanzania bilioni 5.4.

Ameongeza kuwa, mradi wa kuzalisha umeme wa Lupali wenye uwezo wa kuzalisha Kilowati 317 unatekelezwa na Shirika la Benedictine Sisters of St. Gertrud Convent Imiliwaha.
Aidha, fedha zilizotolewa na REA zimewezesha ujenzi wa kituo cha uzalishaji wa umeme na miundombinu ya usambazaji kwenye kituo cha Imiliwaha Sisters Convent pamoja na vijiji vya jirani vya Boimanda, Kitulila na Matola sambamba na kuwezesha tafiti za mradi huo.
Vile vile utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 99 ambapo kazi zilizotekelezwa hadi sasa ni pamoja na ujenzi wa kizuizi cha maji na mtaro wa kupitisha maji ya mafuriko ambao tayari umekamilika.
Naye, Mwenyekiti wa TEF, Bw. Deodatus Balile ameipongeza REA kwa kuweka kiasi kikubwa cha fedha takribani shilingi bilioni 5.4 za kuendeleza na kutekeleza mradi huo ambao unakwenda kuongeza ubora na upatikanaji wa umeme mkoa wa Njombe.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi Sista Imakulata Mlowe, amesema kuwa mara baada ya mradi kukamilika, umeme utakaozalishwa utauzwa moja kwa moja kwa TANESCO ambapo tayari mkataba wa kuuziana umeme umeshasainiwa.
Ameongeza faida za mradi utakapokamilika utaongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wananchi kwa matumizi ya nyumbani na biashara na kupinguza matumizi ya nishati isiyo rafiki na mazingira.
Ziara hiyo ya TEF mkoani Njombe imelenga kupitia utekelezaji wa miradi ya REA inayotekelezwa katika huo sambamba na kupitia maendeleo ya waendelezaji wadogo wa miradi ya kuzalisha umeme hapa nchini na kupatiwa ufumbuzi.








