Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Chalinze
Mgombea ubunge wa Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ridhiwani Kikwete, amesema kuwa endapo wananchi watakipa tena chama hicho ridhaa katika uchaguzi mkuu, serikali ya CCM itahakikisha upatikanaji wa maji kwa asilimia 100 na kufikia zaidi ya kaya 300,000 ndani ya jimbo hilo.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni uliofanyika Septemba 15, 2025 katika viwanja vya Mdaula, Chalinze, Ridhiwani alisema mpango huo utalenga kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi moja kwa moja majumbani, badala ya kutegemea vioski kama ilivyozoeleka.
Alieleza kati ya mwaka 2015 hadi 2020 huduma ya maji ilikuwa ikipatikana kwa asilimia 54 sawa na kaya 76,096.

Hata hivyo, kwasasa kiwango hicho kimeongezeka na kufikia kaya 95,930, sawa na asilimia 92.
Alisema kazi kubwa itakayofanyika katika miaka miwili ya mwanzo ni kuhakikisha upatikanaji wa maji unakamilika kwa asilimia 100, hatua itakayowanufaisha zaidi ya kaya 300,000.
Katika hotuba hiyo, Ridhiwani pia aliwataka wananchi wa Chalinze kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025, kumpigia kura Rais Samia Suluhu Hassan, akisema kuwa ni njia ya kumheshimu kwa kazi kubwa ya maendeleo aliyofanikisha katika kipindi chake cha uongozi.
Alisema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia, Halmashauri ya Chalinze imeongeza makusanyo ya mapato kutoka Shilingi bilioni 9.5 hadi kufikia bilioni 22.3 fedha ambazo zimeelekezwa moja kwa moja katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo jimboni humo.

Kwa mujibu wa Ridhiwani atahakikisha vituo vinne vya mabasi, ikiwemo Kiwangwa, vinakamilika, ujenzi wa hoteli ya nyota nne, kuweka taa za barabarani 500, pamoja na kujenga madarasa 440 katika shule za awali na msingi.
Aliongeza kuwa nyumba 73 za walimu zitajengwa, pamoja na shule mpya 12 za msingi na sekondari 5.
Aliahidi ujenzi wa majengo sita ya TEHAMA, ununuzi wa viti na meza 2,000 kwa shule za sekondari, ujenzi wa mabweni 12 ya wavulana, mabwalo 9 (manne kati ya hayo yako hatua mbalimbali), vituo vya afya 5 na zahanati 21.

Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Pwani, Zainab Vullu, alimnadi Ridhiwani kwa wananchi wa Chalinze na kusisitiza kuwa ushindi wa CCM utahakikisha mwendelezo wa utekelezaji wa ilani yenye matokeo kwa wananchi.
“Tuchague viongozi wanaotujali, Tujitokeze kwa wingi Oktoba 29, tumchague Ridhiwani, wagombea wetu wa udiwani, na Urais Dkt. Samia, maendeleo hayaji kwa bahati, yanahitaji maamuzi sahihi,” alisema Vullu.
