Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz, ameibuka hadharani na kumshutumu vikali aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba Hamfrey Polepole ambaye hivi karibuni alitangaza kujiuzulu wadhifa wake wa kidiplomasia na kuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika mahojiano yaliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Rostam Aziz alisema hana sababu ya kumheshimu mtu ambaye hana historia yoyote ya uongozi ndani ya chama, akisisitiza kuwa balozi huyo “aliibuka tu” mwaka 2015 na kupewa nafasi ya kuwa Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi bila kuwa na mchango wa msingi wala historia ndani ya chama hicho tawala.
“Huyu mtu hana historia yoyote ndani ya CCM. Aliibukia tu 2015, akapewa cheo kikubwa, lakini hajawahi kuwa kiongozi wa ngazi yoyote ndani ya chama kabla ya hapo. Hawa ndiyo madhara ya kuwapa vyeo watu wasiostahili – wanaanza kuropoka maneno wasiyoyajua,” alisema Rostam
Kauli hiyo imezua mijadala mitandaoni huku wengine wakimtazama Rostam kama mtetezi wa misingi ya uongozi wa chama, huku wengine wakihisi kwamba anaendeleza vita ya maneno dhidi ya watu wanaoamua kukosoa au kuondoka CCM na kuelekea upinzani au kujitokeza kama wakosoaji wa wazi wa Serikali.
