Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wakati mataifa mbali mbali duniani yakitoa kipau mbele kwa wananchi wake kumiliki uchumi kupitia upendeleo maalum kwenye biashara na uwekezaji, Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), imempongeza mfanyabiashara maarufu nchini Rostam Aziz kwa uwekezaji wake WA ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Rais TCCIA Bw. Vicent Minja alimpongeza Rostam kwa uwekezaji wake aliofanya na ambao anaendelea kuufanya ndani na nje ya nchi, huku akiishauri Serikali kutunga Sheria maalum itakayotoa upendeleo kwa wazawa.

“Watanzania wanaweza na ndugu Rostam Azizi ni mfano mzuri na wa kuigwa. Rostam amewekeza siyo tu ndani ya nchi bali hata nje ya nchi. Uwezaji wake unainufaisha nchi kupitia ajira, kodi,” alisema rias huyo
Alitaja uwekezaji wa Rostam Aziz kupitia Taifa Gas iliyowekeza pia Kenya,Uganda, Zambia na Malawi Kampuni ya Bia (TBL), pamoja na kununua hisa za TANCOAL na mgodi wa almasi wa Petra.
“TCCIA inatoa pongezi maalum kwa Rostam Aziz kwa hatua zake za kizalendo, alisema na kusisitiza kwamba ununuzi wa hisa za TANCOAL na mgodi wa Petra ni mfano bora wa wazawa kushika hatamu katika sekta za kimkakati.
Tunaipongeza Serikali kwa kuvutia wawekezaji wa ndani na wa nje, lakini bado tunakabiliwa na changamoto ya ushiriki mdogo wa Watanzania katika miradi ya kimkakati,” alisema Bw. Minja. “Ni muhimu sasa kuanzisha mifumo ya kisheria itakayolinda maslahi ya wananchi wa kawaida.”

Bw. Minja alitaja mifano ya Sera ya Uwezeshaji wa Kiuchumi kwa Weusi nchini Afrika Kusini (Black Economic Empowerment) na usimamizi wa rasilimali nchini Urusi baada ya enzi ya Usovieti kama mifano inayoonyesha jinsi mikakati ya kitaifa ya makusudi inavyoweza kuinua wananchi.
“Uchumi wa taifa hauwezi kuwa wa kizalendo kama hauwapi fursa wananchi wake. Uwekezaji unaowajumuisha Watanzania ndiyo uwekezaji bora zaidi,” alisema Bw. Minja.
TCCIA ilitambua uwepo wa sheria kama Sheria ya Ushiriki wa Watanzania (Local Content Act), Sheria ya Ununuzi wa Umma (Public Procurement Act), na Kanuni za Madini kuhusu Ushiriki wa Watanzania za mwaka 2018, ambazo zimeweka msingi wa kulinda maslahi ya wananchi.

Hata hivyo, TCCIA ilisisitiza kuwa utekelezaji wa sheria hizo unapaswa kuimarishwa ili kuhakikisha Watanzania hawabaki watazamaji katika uchumi wao wenyewe.
Aidha, Bw. Minja alitoa mifano ya mafanikio kutoka sekta ya michezo na viwanda, akiwapongeza viongozi wa sekta binafsi wakiwemo Azam Media, NBC, MO Dewji, GSM, CRDB, Said Salim Bakhresa, Ally Awadh, Subhash Patel na Rostam Aziz.
