Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi Salim Morcase, amewataka waandishi wa habari mkoani humo kuzingatia weledi, miiko na kanuni za taaluma ya uandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao, hususan katika kipindi cha kuelekea uchaguzi.

Akizungumza Septemba 3, 2025, katika ukumbi wa ofisi yake, wakati wa semina maalum iliyoandaliwa kwa waandishi wa habari kuhusu “Wajibu wa Waandishi wa Habari na Jeshi la Polisi katika Kulinda Usalama Wakati wa Uchaguzi”, Kamanda Morcase alieleza kuwa waandishi ni wadau muhimu katika mchakato mzima wa uchaguzi, hivyo wanapaswa kuelimisha umma kuhusu haki na wajibu wao wa msingi, ikiwemo kushiriki kupiga kura.

Aidha, aliwasisitiza kuepuka matumizi ya lugha isiyo ya staha au yenye viashiria vya uchochezi ambayo inaweza kusababisha taharuki katika jamii.

Kwa upande wake, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Haway Amnay, aliwataka waandishi kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayosimamia tasnia ya habari nchini, ikiwemo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya Huduma za Habari, Kanuni za Maadili ya Waandishi wa Habari, Sheria ya Makosa ya Mtandao, pamoja na miongozo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Naye Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoa wa Pwani, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Nemes Kavishe, aliwasihi waandishi kuhakikisha usalama wao binafsi wakati wa kutekeleza majukumu yao kipindi hiki cha uchaguzi.

Akizungumza kwa niaba ya waandishi wa habari waliokuwepo, Herieth Kiama kutoka gazeti la Daily News, alilishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa kutambua mchango wa vyombo vya habari katika masuala ya usalama na amani.