Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

JESHI la Polisi mkoani Pwani, kupitia kitengo cha usalama barabarani, limekamata jumla ya makosa 74,446 ya usalama barabarani na kukusanya faini za papo kwa papo zenye thamani ya Sh. bilioni 2.233.

Aidha, jeshi hilo, kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani, linaendelea kudhibiti msongamano wa magari katika Barabara Kuu ya Dar es Salaam-Morogoro, foleni ambayo inatokana na ongezeko la magari na miundombinu finyu ambayo serikali ipo mbioni kupanua barabara hiyo ili kupunguza kadhia hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia Septemba hadi Novemba 2025 katika mkutano uliofanyika Ukumbi wa Mikutano, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Pwani, Kamanda wa Polisi mkoani Pwani (ACP) Salim Morcase alisema ,madereva 38 wamefungiwa leseni zao kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani.

Morcase alieleza ,elimu ya usalama barabarani ilitolewa katika shule za msingi 42, shule za sekondari 36 na vyuo vya udereva viwili , wanafunzi 3,234 ,madereva na abiria katika stendi na vijiwe 54 vya bodaboda na watembea kwa miguu.

Aliongeza kuwa kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka, wanawakumbusha wananchi wanaotarajia kusafiri kwenda mikoani kwa kutumia vyombo vya moto, kutokata tiketi kwenye mabasi ambayo yameshajaza.

“Wakati abiria wakishindwa kufuata sheria, mshtakiwa wa kwanza atakuwa abiria mwenyewe aliyesimama bila tiketi”.

“Katika Mkoa wa Pwani tupo makini, yeyote anayepita Barabara Kuu ya Morogoro atakaguliwa, na endapo ukibainika kwenda kinyume na sheria za usalama barabarani, sheria itachukua mkondo wake kulingana na kosa atakalokutwa nalo,” alifafanua Morcase.

Vile vile, alisema kuwa katika operesheni hizo wamefanikiwa kukamata watuhumiwa 203 waliokutwa na makosa mbalimbali.

Kadhalika, Morcase alieleza kati ya makosa yaliyoripotiwa kwenye vituo vya polisi, jumla ya kesi 47 zimefikishwa mahakamani na kupata ushindi, huku watuhumiwa 53 wakihukumiwa vifungo mbalimbali, ikiwemo vifungo vya maisha kwa makosa ya kubaka na kulawiti.