Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Ngara
Katika kile kinachoonekana kuwa kiu ya kuwatumikia Wanangara na kuifanya Ngara kuwa kubwa kwenye ramani ya dunia, Hilali Alexander Ruhundwa amejitosa kuwania nafasi ya ubunge jimbo la Ngara kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akielezea maono yake mara baada ya kurejesha fomu za kuomba ridhaa ya CCM kuwa mbunge wa Jimbo la Ngara, Ruhundwa ameeleza kwa ufupi atakayoyafanya endapo CCM itamwamini kupeperusha bendera katika Uchaguzi Mkuu ujao mwezi Oktoba na kupata ushindi:

Mosi, Ruhundwa amesema anaamini zaidi katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kila sekta kuleta maendeleo kutokana na ukuaji wa teknolojia duniani.
Elimu: Kuhakikisha kila shule ya sekondari ya kata inakuwa na darasa la TEHAMA. Kushawishi vyuo vikuu ndani na nje ya nchi kujenga matawi ya vyuo vyao ndani ya Ngara. Kuhakikisha Ngara inazalisha wataalam wa teknolojia na wahandisi. Kuongeza walimu/wakufunzi na vifaa vya kutosha.
Vituo vikubwa vya TEHAMA: Kuhakikisha Ngara ina vituo viwili vikubwa vya TEHAMA kuwapa fursa vijana wabunifu na wananchi wote kupata ujuzi na kutumia fursa zilizopo za teknolojia duniani.
Viwanda: Kushawishi na kuleta wawekezaji kuanzisha viwanda ndani ya Ngara na kuzalisha bidhaa mbalimbali. Kuwa na kiwanda cha kuzalisha vifaa tiba na vifaa vingine vya afya hasa wakati huu nchi za Afrika zinapoanza kujitegemea baada ya nchi za Magharibi kukata misaada kwenye sekta ya afya.
Kilimo: Kuleta wataalam toka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia kupima afya ya udongo na kushauri mazao ya kulima kwa kutumia njia za kisasa. Kuongeza mazao ya biashara na chakula ndani ya Ngara.
Ufugaji: Kuwa na ufugaji wa kisasa na kuongeza idadi ya mifugo hivyo kuzalisha malighafi za kutosha kama nyama, ngozi na maziwa vitakavyotmika kwenye viwanda ndani ya Ngara.
Bandari ya nchi kavu: Kushawishi serikali na sekta binafsi kujenga bandari ya nchi kavu itakayohudumia nchi jirani na Ngara.
Ushirikiano wa Sekta Binafsi na Serikali: Kuishauri na kuishawishi serikali kushirikisha sekta binafsi kujenga miundombinu na kutoa huduma kwa wananchi hasa maji nk.
Michezo: Kusaka na kuibua vipaji vya Wanangara na kuwa na timu za wanawake na wanaume zenye kuleta ushindani kitaifa na kimataifa.
Utamaduni: Kuwa na makumbusho ya utamaduni wa Wanangara. Kuzalisha nyimbo na vipindi vinavyoelezea mila na desturi za Ngara na kuitangaza Ngara kitaifa na kimataifa na kuvutia utalii. Hii itasaidia kuondoa usumbufu wa Idara ya Uhamiaji na mtazamo wa walio wengi kuhusu uraia wa watu wa Ngara.
Baraza la Wazee la Ngara: Kuwa na Baraza la Wazee wa Ngara lenye nguvu na ushawishi kushauri na kupendekeza vipaumbele vya maendeleo ya Ngara. Baraza hili pia kuonya na kurudisha kwenye mstari viongozi watakaokuwa wanakengeuka.
Mahusiano mema: Kuwaleta Wanangara na kuwaunganisha pamoja katika kuijenga Ngara. Kuwa na mazingira rafiki kwa wazawa waliopo nje ya Ngara kurudi kuwekeza nyumbani.
Pamoja na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na Dira ya Taifa, Ruhundwa atahakikisha kuwa hayo yote hapo juu yanatekelezeka kwa ufanisi na kuleta tija kwa Ngara.

