Na Dotto Kwilasa,JemhuriMedia,Dodoma

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika, Dkt. Dickson Chilongani, ameiomba Serikali kuongeza jitihada katika kushughulikia kero zinazowakabili wananchi, hususan vitendo vya rushwa, ukiritimba na kunyimwa haki katika baadhi ya taasisi na ofisi za umma.

Akizungumza katika ibada ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Paulo wa Msalaba jijini Dodoma, Dkt. Chilongani amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, ikiwemo ongezeko la mishahara kwa watumishi wa umma, bado wananchi wengi wanakumbana na changamoto zinazopunguza furaha na ustawi wao.

Ameeleza kuwa miongoni mwa kero zinazoendelea kujitokeza ni vitendo vya rushwa vinavyofanyika waziwazi, ambapo baadhi ya watumishi hudaiwa kuomba kile kinachoitwa ‘facilitation’ ili kutoa huduma.

“Tunashukuru mwaka jana mishahara iliongezwa,lakini bado kuna kero nyingi kwenye maofisi,ukiritimba, kunyimwa haki na rushwa bado ni changamoto,Sasa hivi ‘facilitation’ zinaombwa waziwazi,” amesema,

Ameongeza kuwa hali hiyo imekuwa kikwazo kwa wananchi wanaohitaji huduma, akieleza kuwa hata taasisi za dini zimekuwa zikikumbana na hali hiyo wanapofuatilia masuala mbalimbali muhimu.

“Unamtuma mfanyakazi ashughulikie suala muhimu anakwambia Baba Askofu tukienda wanatuomba facilitation,hawaoni aibu hata kuliomba Kanisa litoe facilitation,tuiombe Serikali itupie macho kero hizi ili Watanzania waishi kwa furaha,” amesisitiza.

Hata hivyo, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano nchini, akibainisha kuwa mafanikio hayo ni msingi muhimu wa maendeleo, lakini bado jitihada zaidi zinahitajika ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wote.

Aidha, Dkt. Chilongani ameitaka jamii kushiriki kikamilifu katika kujenga taifa lenye maadili mema, akisisitiza kuwa kipindi cha Pasaka kinapaswa kuwa chachu ya matumaini, mabadiliko chanya na kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi.