Na Albano Midelo, JamhuriMedia, Ruvuma

Katika kipindi kifupi cha miezi mitatu tu, Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma imeandika historia mpya ya uwajibikaji, uwazi na vita dhidi ya vitendo vya rushwa, ikiongozwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Ruvuma.

 Mabadiliko haya makubwa si tu yanatoa matumaini mapya kwa wananchi bali pia yanaweka alama isiyofutika ya jinsi Taasisi za umma zinavyoweza kuwa chombo cha kweli cha maendeleo.

Katika mazungumzo maalum na wanahabari yaliyofanyika ofisini kwake Mahenge mjini Songea, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma, Janeth Haule, alifungua ukurasa wa mafanikio ya kushangaza yaliyoanza kuonekana katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025,kipindi kifupi kilichozaa matokeo makubwa.

Fedha Zilizoibwa Zarejeshwa Benki

Katika ufuatiliaji wake wa karibu, TAKUKURU iligundua kuwa shilingi 9,205,158.44 ambazo ni mapato halali ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea kutoka vyanzo mbalimbali, zilikuwa zimekusanywa na mawakala kupitia mifumo ya kielektroniki lakini hazikuwasilishwa benki kama ilivyopaswa.

Kwa weledi na msimamo wa kuhakikisha fedha za umma haziishii mifukoni mwa watu wachache, TAKUKURU iliingilia kati na kuhakikisha kuwa fedha hizo ziliwasilishwa benki kikamilifu.

Hili ni tukio linaloonesha jinsi ambavyo taasisi hiyo imekuwa chombo hai cha kusimamia rasilimali za wananchi kwa maslahi ya umma.

Makusanyo Yapanuka Kwa Kasi ya Ajabu

Athari chanya za ufuatiliaji wa TAKUKURU hazikuishia kwenye urejeshwaji wa fedha pekee.

 Idara mbalimbali ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea zikiwemo Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Biashara na Ardhi na Maliasili zilishuhudia ongezeko la makusanyo ya mapato kutoka chini ya asilimia 50 hadi kufikia asilimia 102.6, kupitia mfumo wa kielektroniki.

Ni wazi kwamba mfumo huu unavyotumiwa vizuri, si tu unazuia upotevu wa mapato bali pia unakuza uwajibikaji na nidhamu ya matumizi ya fedha.

Miradi milioni 29 Yarejeshwa Katika Mstari

Katika hatua nyingine ya kustaajabisha, TAKUKURU ilitoa ushauri wa kitaalamu wa kurekebisha mapungufu katika miradi mitatu yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 29.9. Miradi hiyo inayohusu sekta ya Miundombinu, Kilimo na Fedha ilikuwa kwenye hatari ya kutofikia malengo yake, jambo ambalo lingesababisha hasara kwa Serikali na wananchi.

Hata hivyo, mapungufu hayo yalirekebishwa haraka, hatua iliyosaidia fedha hizo kutumika kama ilivyokusudiwa na kuwanufaisha walengwa kwa ufanisi mkubwa.

Vikao, Warsha na Maazimio 16 Dhidi ya Rushwa

Katika juhudi za kimkakati, TAKUKURU ilifanya uchambuzi wa mifumo mitatu na warsha tatu na wadau mbalimbali kwa lengo la kuziba mianya ya rushwa.

Vikao hivyo vilizaa maazimio 16 yenye mwelekeo wa kubadili utendaji wa taasisi za umma na kuimarisha usimamizi wa rasilimali.

TAKUKURU Rafiki Yatikisa Kata 12

Kupitia programu ya TAKUKURU Rafiki, taasisi hiyo ilifika kwenye kata 12, ambako jumla ya kero 118 ziliibuliwa kutoka kwa wananchi. Cha kufurahisha, kero 89 tayari zimetatuliwa huku kero 29 zikiendelea kufanyiwa kazi.

Hili ni jibu la wazi kwa madai ya muda mrefu kuwa wananchi hawana pa kupaza sauti TAKUKURU imekuwa jicho na sikio lao.

Elimu kwa Umma Yaleta Matokeo

Katika eneo la uelimishaji, TAKUKURU haikubaki nyuma. Imeendesha semina 24, mikutano ya hadhara 26, maonesho 6, pamoja na vipindi vya redio 3 vilivyolenga kuwaamsha wananchi kuhusu madhara ya rushwa na wajibu wao wa kuikataa. Klabu za wapinga rushwa 53 zimeimarishwa na makala mbili zimeandaliwa kwa ajili ya vyombo vya habari.

Mafanikio Katika Uchunguzi na Mashtaka

Katika kipindi hicho, malalamiko 100 yalipokelewa, ambapo 80 yalihusu rushwa na 20 hayakuhusu rushwa. Kesi nne zilifikishwa mahakamani, na katika kesi  tatu zilizotolewa hukumu, Jamhuri imeshinda zote ishara kwamba ushahidi uliwasilishwa kwa weledi na kazi ya uchunguzi ilifanyika kwa umakini mkubwa.

Wito Maalum kwa Uchaguzi Mkuu 2025

Kwa kuhitimisha, Janeth Haule ametoa rai kwa wananchi wote kujiandaa na kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, akisisitiza kuwa “Rushwa haina nafasi katika uchaguzi huru na wa haki.

Wananchi wachague viongozi waadilifu wasiotokana na rushwa, ili Taifa letu liendelee kulindwa na kuletwa katika njia ya maendeleo ya kweli.