Rais wa Kenya William Ruto Jumatano amelaani mauaji ya mwanablogu mmoja nchini humo yaliyotokea katika seli ya Polisi alimokuwa akishikiliwa, tukio lililozusha hasira miongoni mwa Wakenya.
Awali polisi ya Kenya ilikuwa imesema kuwa Albert Ojwang, aliyekamatwa kwa chapisho aliloliweka kwenye mtandao wa kijamii akimtuhumu naibu inspekta mkuu wa polisi nchini humo, alifariki kwa kukigongesha kichwa chake ukutani.
Ila madaktari wa upasuaji hapo Jumanne walisema kuwa hakuna uwezekano kwamba Ojwang alijitoa uhai, baada ya kufanya upasuaji na kuweka wazi ripoti ya upasuaji huo.
Mpasuaji wa serikali, mmoja kati nya watano walioufanyia upasuaji wa Ojwang,aliwaambia waandishi wa habari Jumanne kuwa, “uwezekano wa Ojwang kujijeruhi mwenyewe ulikuwa mdogo.”
“Tukio hili la kifo mikononi mwa polisi linavunja moyo na halikubaliki,” alisema Ruto.
Ametoa wito kwa polisi kutoa ushirikiano kikamilifu ili kuhakikisha “uchunguzi wa haraka, wenye uwazi na wa kuaminika.”
“Nataraji kikamilifu kuwa kilichomsibu Ojwang kitajulikana kwa wakati ufaao na haki itatendeka,” alisema Ruto.
Kifo cha Ojwang aliyekuwa na umri wa miaka 31 kinakuja wakati ambapo Kenya inaadhimisha mwaka mmoja tangu maandamano makubwa ya vijana ya kupinga nyongeza ya ushuru yaliyosababisha vifo vya takriban vijana 60 na wengine wengi kupotea.

