Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Rufiji

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Mohamed Mchengerwa, ameshuhudia hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa miradi ya maji katika vijiji vya Mloka, Mbunju Mvuleni na Ndundutawa, itakayonufaisha wananchi 16,593 na kuondoa kero ya muda mrefu ya ukosefu wa maji safi.

Akitoa taarifa ya miradi hiyo, Mei 7,2025 Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Rufiji, Mhandisi Alkam Sabuni, alisema miradi hiyo itatekelezwa kwa gharama ya sh.791,068,682.56 na inatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi minne, kuanzia Juni hadi Oktoba 2025.

“Kupitia miradi hii, upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo haya utaongezeka kutoka asilimia 86.6 ya sasa hadi kufikia asilimia 97.3,” alifafanua Sabuni.

Alisisitiza kwamba huu ni uwekezaji wa maana kwa afya na ustawi wa jamii za vijijini.

Kwa mujibu wa Sabuni, RUWASA Rufiji kwa sasa inatoa huduma katika jumla ya vijiji 38 vyenye wakazi 157,412, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Kwa upande wake, Mchengerwa alieleza utekelezaji wa miradi hiyo ni mafanikio makubwa kwa wananchi wa Rufiji, hususan wale waliokuwa wakilazimika kutumia maji ya Mto Rufiji kwa shughuli za kila siku.

“Leo tumeandika historia, tumefunga ukurasa wa mateso ya muda mrefu kwa wananchi wetu,mkandarasi hana sababu ya kuchelewa — tunataka kazi ianze mara moja,” alisisitiza Mchengerwa .

Wananchi wa vijiji hivyo walishukuru kwa matumaini makubwa ya kuondokana na changamoto ya maji ambayo kwa muda mrefu imekuwa kikwazo kwa maendeleo na afya ya jamii.